Elimu zaidi inahitajika utoaji mimba usio salama

“SIKUA na sh 150,000 niliyotakiwa kulipa kwenye kituo kimoja cha afya baada ya kudondoka na ujauzito wangu kutoka, ” anasema Grace Chacha (sio jina lake halisi) 19, ambaye amekuwa mlemavu baada ya kukatwa miguu na vidole tisa mkononi.

Grace kwa sasa ni mlemavu, alilazimika kukatwa viungo vyake baada ya kupata uambukizi katika kizazi uliosababisha kuoza kwa kizazi na maambukizi kusambaa hadi kwenye miguu na vidole, baada ya kuchelewa kupata huduma ya kusafishwa mimba ilipoharibika.

Huyo ni Grace mmoja lakini wapo akina Grace wengi, ambao wanaishi na majeraha baada ya kuharibikiwa mimba na kukosa matibabu stahiki kutokana na wengi kutokuwa na uelewa wa huduma wanayotakiwa kupata baada ya mimba kuharibika kuwa  hutolewa bure katika vituo vya afya vya mama na mtoto.

Serikali kwa kushirikiana na taasisi zisizo za kiserekali zimekuwa zikiendesha mafunzo  ya huduma baada ya mimba kuharibika ‘Comprehensive Post Abortion Care’ (CPAC),  ambayo yamesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza vifo na athari kwa wanawake wanaoharibikikiwa na ujauzito.

Pia yamechangia kuongeza ufanisi kwa baadhi ya watoa huduma katika zahanati mbalimbali nchini na sasa huduma hiyo kupatikana  ndani ya vituo vya afya kwa kila kata

Kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2016 zilizotolewa na Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMRI) kwa kushirikiana na Chuo Kikuu Cha Afya na Sayansi Shirikishi-Muhimbili (MUHAS) na Taasisi ya Guttmacher ya Marekani inaonesha kuwa karibia wanawake 67,000 walitibiwa katika vituo vya afya kwa ajili ya matatizo yanayotokana na utoaji mimba usio salama kwa mwaka 2013 nchini Tanzania.

Hata hivyo, karibu wanawake wengine 100,000 ambao walipata matatizo yaliyohitaji tiba katika kituo cha afya hawakupata matibabu waliyohitaji.

Hospitali za rufaa na mikoa hutibu wagonjwa wengi wanaopata huduma baada ya kuharibika kwa mimba; kwa wastani, kila moja ilitibu karibia wagonjwa 1,140 na 710 kwa mtiririko ndani ya mwaka 2013.

Kwa wastani, chini ya vituo vya afya nane hutoa huduma baada ya kuharibika kwa mimba kwa kila wanawake 100,000 nchini Tanzania.

Zanzibar inatoa huduma zaidi, ikiwa na vituo zaidi ya 10 kwa wanawake 100,000, wakati ukanda wa Mashariki una vituo vichache vya huduma hii chini ya vituo sita kwa kila wanawake 100,000.

Viwango vya tiba kwa matatizo yatokanayo na kuharibika na utoaji mimba hutofautiana kwa kiasi kikubwa na kikanda, hii ni kwa sababu ya usambazwaji usiokuwa wa usawa wa watoa huduma baada ya kuharibika kwa mimba.

Akizungumzia hilo, muwezeshaji wa Kitaifa wa Mafunzo ya mama baada ya mimba kuharibika (CPAC) chini ya Wizara ya Afya, muunguzi David Ponela kutoka Hospitali ya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam, anasema serikali kushirikiana na wadau inapambana kujua sehemu gani kuna uhitaji zaidi ili kutoa kipaumbele zaidi kwa kuwapelekea wahudumu pamoja na mafunzo

“Huduma ya CPAC ni bure kwa mama hakuna gharama yoyote, na huduma hii ipo kwenye vituo vyote vya afya katika ngazi ya wilaya na kata, serikali inajitaidi kupelekea huduma hii nchi nzima ili kupunguza vifo vitokanavyo na ujauzito,” anasema Ponela.

Anasema ni muhimu kuhusisha takwimu kwenye CPAC kwa sababu wizara bado inapambana kusaidiana na wadau kujua sehemu gani kuna uhitaji, ili kuwapelekea huduma na kutoa mafunzo zaidi kwa watoa huduma.

Amesema; “Ndio maana tunawafundisha watoa huduma pia namna ya kuandika takwimu hii husaidia kutambua sehemu yenye uhitaji zaidi na kusaidia sehemu husika.”

Hata hivyo, Ponela amesema changamoto kubwa ambayo ipo ni usimamizi kwa watoa huduma ambao baadhi yao hawafahamu kuwa anatakiwa kuijaza fomu hiyo mara kwa mara.

“Ili kupunguza changamoto hiyo tumeendelea kutoa mafunzo kwa waratibu wakuu wa kila wilaya na kata nchini ili nao wakatoe elimu zaidi kwa  wahudumu waliopo chini yao,” amesema Ponela.

Naye daktari bingwa wa magonjwa ya kina mama na Mkufunzi wa Kitaifa wa Mafunzo ya CPAC, Dk Elias Kuyamba, akizungumza na HabariLEO anasema CPAC inasaidia kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi, au mama kuharibikiwa na mimba.

“Baada ya kufanya uchunguzi ilionekana vifo vya wajawazito vinazuilika, kwa kuwa vinazuilika tukafikiri kutengeneza miongozo jumuishi ambao unatumika nchi nzima.

“Mama ambaye ameharibikiwa na mimba kwa umri wowote ajue unamtibu kwa namna gani ndio sababu ya kutengeneza mwongozo, lengo la wizara ni kuipeleka kwa kila kituo ili watoa huduma wausome na kuielewa ili wakipata ‘case’ ya nama hiyo, wajue namna ya kumtibu mama ili kupunguza vifo.

Amesema kupunguza maumivu ya kumsafisha mama baada ya mimba kuharibika, kuna kitabu cha kukusanya kumbukumbu kinaitwa MTUHA NAMBA 17,  ambacho kimetoa mgawanyo wa aina ya matibabu anayopaswa kupatiwa mgonjwa.

Uimarishaji huduma/uzazi wa mpango

Ili kupunguza utoaji mimba usio salama na vifo vya wajawazito na majeraha yanayohusishwa na utoaji mimba, serikali inapaswa kupanua zaidi upatikanaji wa huduma za uzazi wa mpango, ili kuzuia mimba zisizotarajiwa, na kupanua upatikanaji wa huduma baada ya kuharibika kwa mimba.

Kwa mujibu wa takwimu za Muhas, Nimri na Guttmacher, Tanzania ni kati ya nchi zenye uwiano wa juu wa vifo vya wajawazito duniani 410  kwa kila  vizazi hai  100,000, na utoaji mimba usio salama ni moja kati ya sababu zinazoongoza.

Utoaji mimba usio salama unachangia zaidi ya theluthi moja ya wanaolazwa hospitalini kutokana na matatizo yanayohusiana na mimba na takribani robo moja ya vifo vya uzazi.

Sheria na sera ya utoaji mimba nchini Tanzania inang’ata na kupuliza. Sheria ya makosa ya jinai huidhinisha utoaji mimba, ili kuokoa maisha ya mwanamke, lakini haijaweka wazi kama utaratibu huu utalinda afya ya mwili na akili ya mwanamke.

Hofu ya kushtakiwa, ambayo ipo kwa wanawake na watoa huduma ya afya pia, husababisha wanawake watoe mimba kwa siri kwa njia ambazo mara nyingi huwa si salama.

MATUKIO YA UTOAJI MIMBA

Inakadiriwa kuwa, mimba 405,000 zilitolewa ndani ya mwaka 2013 nchini Tanzania. Idadi hii ni kiwango cha utoaji mimba 36 kwa kila wanawake 1,000 wenye umri kati ya miaka 15 – 49 na uwiano wa utoaji mimba 21 kwa kila watoto 100 wanaozaliwa wakiwa hai.

Kiwango cha utoaji mimba ni sawa na wastani wa kiwango cha kanda ya Afrika Mashariki kwa ujumla (36 kwa kila wanawake 1,000) na juu kidogo kuliko kiwango cha nchi za Kusini mwa Sahara (31).

Viwango vya utoaji mimba hutofautiana sana kwa ukanda, kutoka 11 kwa wanawake 1,000 kwa Zanzibar hadi 47 kwa Nyanda za Juu Kusini na 51 kwa Kanda ya Ziwa.

Ukanda wa Ziwa na Nyanda za Juu Kusini huwa na viwango vya juu vya matibabu kwa matatizo yatokanayo na utoaji mimba pia.

Mwaka 2013, katika nchi nzima, asilimia 15 ya mimba zilitolewa, asilimia 52 katika uzazi uliokusudiwa, asilimia 18 katika uzazi usiokusudiwa na asilimia 15 katika mimba zilizoharibika.

Mgawanyo huu hutofautiana kwa maeneo kwa mfano, uwiano wa mimba zilizotolewa ni kati ya asilimia 6 kwa Zanzibar hadi asilimia 18 kwa Nyanda za Juu Kusini.

SABABU ZA VIWANGO VYA UTOAJI MIMBA

Sababu kadhaa kueleza tofauti katika viwango vya utoaji mimba kwa ukanda: tofauti katika idadi ya watoto ambayo wanawake wanataka kuwa nao, tofauti katika tendo la kujamiiana na matumizi ya uzazi wa mpango, na tofauti katika uwezekano wa wanawake wa kutegemea utoaji mimba katika tukio la mimba zisizotarajiwa.

Mwanamke mmoja kati ya watano wenye umri kati ya miaka 15 hadi 49 nchini Tanzania wanataka kuchelewesha au kusitisha kuwa na watoto, lakini hawatumii njia yoyote ya uzazi wa mpango. Kundi hili la wanawake huchukuliwa kama lenye mahitaji yasiyofikiwa ya uzazi wa mpango.

Akizungumzia hali hiyo, daktari wa magonjwa ya wanawake kutoka mkoani Mwanza, John Chacha anasema ili kuhimarisha huduma ya mama baada ya kuharibikiwa mimba, vituo vya afya katika ngazi zote lazima viwe na dawa muhimu za kutosha, vifaa vya kutolea huduma za msingi za baada ya kuharibika kwa mimba, na watoa huduma wa kawaida wanapaswa wapewe mafunzo zaidi ya kutoa huduma hizo.

Anasema, huduma baada ya kuharibika kwa mimba zitolewe sambamba na huduma za uzazi wa mpango kwa sababu wagonjwa wanaopokea huduma baada ya kuharibika kwa mimba hupokea sana ushauri nasaha juu ya uzazi wa mpango.

Chacha anasema tafiti zimegundua kwamba idadi kubwa ya wagonjwa hao hukubali njia za uzazi wa mpango na kuendelea kuzitumia.

“Huduma baada ya kuharibika kwa mimba inatoa fursa ya kushirikisha wanaume katika uzazi wa mpango: Imeonekana kuwa wanaume wanaokwenda na wapenzi wao kwenye huduma baada ya kuharibika kwa mimba hupokea vizuri  taarifa za uzazi wa mpango ambazo humsaidia yeye na mwenza wake,”  amesema Chacha.

Habari Zifananazo

Back to top button