Endelea kupumzika JPM, Kazi Inaendelea

NI miaka miwili sasa imetimia tangu aliyekuwa Rais wa Serikali ya Awamu ya Tano, Dk John Magufuli afariki dunia kutokana na matatizo ya moyo katika Hospitali ya Mzena iliyopo mkoani Dar es Salaam.

Kifo cha Rais Magufuli kilitokea miezi michache baada ya kushinda Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 uliompa ridhaa ya kuongoza tena nchi kwa kipindi cha pili cha miaka mitano ambacho angekihitimisha mwaka 2025.

Machi 17, 2021 ni siku ambayo Taifa la Tanzania na Watanzania kwa ujumla walijikuta katika simanzi nzito kwa kufiwa na Rais ambaye ni Mkuu wa nchi, Dk Magufuli akiwa madarakani.

Katika kuadhimisha miaka miwili ya kifo chake, ni vyema Watanzania wakakumbuka baadhi ya mambo makubwa ya kimaendeleo ambayo serikali yake imeyatekeleza katika kipindi cha kwanza cha miaka mitano ya utawala wake.

Katika miaka mitano (2015-2020), Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya Awamu ya Tano chini ya Dk Magufuli, ilijitahidi kugusa maisha ya Watanzania kwa upana wake kwa kutekeleza miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya usafirishaji, umeme, maji, elimu, afya na serikali kuhamia rasmi Dodoma.

SERIKALI KUHAMIA DODOMA

Ilikuwa ni wazo la Rais wa Awamu ya Kwanza, Mwalimu Julius Nyerere lililopitishwa kisheria wakati wake kuwa Makao Makuu ya Nchi ni Dodoma na katika uongozi wa Magufuli mwaka 2019 serikali rasmi ilihamia Dodoma baada ya kuzindua Mji wa Kiserikali.

Ofisi za wizara, taasisi na mashirika ya umma, balozi na kampuni binafsi zikaanza kuhamia Dodoma. Ikulu ya Chamwino ikaanza kujengwa ya kisasa yenye mfanano wa ya Magogoni, Dar es Salaam ikiwa na wanyamapori ndani yake. Sasa serikali ipo Dodoma kikamilifu na kazi inaendelea.

RELI YA SGR NA UKARABATI RELI KASKAZINI

Miongoni mwa miradi mikubwa ya usafirishaji ambayo ilitekelezwa na mingine bado inaendelea kutekelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, ni ujenzi wa reli ya kisasa awamu ya kwanza na ya pili kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro na kutoka Morogoro hadi Makutupora mkoani Singida yenye urefu wa kilometa zaidi ya 700 kwa gharama ya takribani Sh trilioni 7.026.

Kipande cha reli hii kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro chenye urefu wa kilometa 300 kinakaribia kukamilika lakini mpaka Juni mwaka 2020, ujenzi wa SGR kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro ulikuwa umefikia asilimia 82 na Morogoro-Makutupora kilometa 422 ulikuwa umefikia asilimia 34.

Hayati JPM

UKARABATI WA RELI

Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Magufuli ilifanikiwa kukarabati reli ya kutoka Dar es Salaam-Tanga-Moshi-Arusha kwa gharama zaidi ya Sh bilioni 14.

BANDARI

Serikali ya Awamu ya Tano pia ilifanya upanuzi wa bandari zake kuu nchini ikiwemo ya Dar es Salaam, Tanga na Mtwara kwa kuziboresha na kuziimarisha ili zihimili ushindani wa kibiashara katika ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika.

Katika Bandari ya Dar es Salaam miongoni mwa maboresho ambayo Serikali ya Magufuli iliyafanya ni pamoja na kujenga gati jipya la kupakulia magari, kuimarisha gati zilizokuwepo, kuongeza kina cha gati hadi kufikia mita 15 kuruhusu meli kubwa za mizigo kutia nanga bila tatizo.

Mkoani Mtwara Serikali ya Awamu Tano ilianza ujenzi wa gati jipya namba mbili kwa gharama ya Sh bilioni 137.4 ambalo limekamilishwa na Serikali ya Awamu ya Sita. Sifa pekee ya gati hili ni kwamba limejengwa mahali ambapo kuna kina kirefu cha maji cha asili kinachofikia mita 13 wakati maji yanapokupwa.

Serikali ya Magufuli pia ilianza ujenzi wa upanuzi katika Bandari ya Tanga ikiwemo kuongeza kina ili meli kubwa za mizigo na mafuta zitie nanga.

Wakati anazindua safari za treni ya abiria kutoka Dar es Salaam hadi Arusha, Rais Magufuli aliweka wazi kuwa kupanuliwa kwa Bandari ya Tanga kutawezesha kuwapunguzia gharama za bidhaa wananchi wa mikoa ya Kaskazini kwa kuwa baadhi ya meli kubwa za mizigo hazitalazimika kwenda Bandari ya Dar es Salaam.

UMEME VIJIJINI NA MRADI JNHPP

Ili kukidhi mahitaji ya umeme pamoja na kujenga uchumi wa viwanda, Serikali ya Awamu ya Tano iliamua kutekeleza ujenzi wa mradi wa Kufua Umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) katika Mto Rufiji mkoani Pwani.

Utekelezaji huu ulizingatia uamuzi mgumu aliochukua Magufuli licha ya kuwepo na vikwazo vingi kutoka mataifa ya nje. Gharama ya zaidi ya Sh trilioni 6 inatumika na ukikamilika utazalisha megawati 2,115.

Sasa Serikali ya Rais Samia inauendeleza na mpaka sasa ujenzi wake umefikia zaidi ya asilimia 80.

Magufuli wakati wake alisema alipoingia madarakani mwaka 2015, vijiji vilivyokuwa na umeme vilikuwa 2,018 kati ya vijiji vyote 12,280 vilivyopo, lakini serikali yake ilifanikiwa kupeleka umeme kwenye vijiji 9,700 na vilibakia vijiji 2,500 ambavyo Serikali ya Rais Samia imevipelekea nishati hiyo.

Ujenzi wa Reli ya SGR ukiendelea.

BOMBA LA MAFUTA

Mradi mwingine mkubwa ambao Serikali ya Rais Magufuli ilianza kuutekeleza ni ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani katika Bandari ya Tanga.

Dk Magufuli aliliambia taifa kuwa mkataba wa ujenzi wa bomba hilo lenye urefu wa kilometa 1,445 ulishasainiwa na ujenzi wake utagharimu Sh trilioni 8. Hivi sasa mradi huu unaendelezwa na Rais Samia aliyekuwa Makamu wa Rais katika utawala wa Magufuli (JPM).

 

Hayati JPM

MELI MPYA

Katika kuhakikisha uchumi wa Tanzania na maisha ya Watanzania yanaboreka, Serikali yake ilitekeleza mradi wa ujenzi wa meli mpya na ya kisasa katika Ziwa Victoria iliyopewa jina la Mv Mwanza Hapa Kazi Tu. Kununuliwa kwa meli hii ni utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2015-2020 ukurasa wa 67 iliyoelekeza kujengwa kwa meli mpya katika Ziwa Victoria.

Ujenzi wa meli hiyo ambao unakamilishwa na Serikali ya Rais Samia, ilielezwa wakati huo kwamba ungegharimu Sh bilioni 89.7 na gharama ya ujenzi wa chelezo ni Sh bilioni 36.4. Kazi inaendelea na iko mwishoni kukamilika kwani meli hii imeshaingizwa majini kwa majaribio.

BARABARA NA MADARAJA

Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kupitia Toleo lake maalumu kwenye gazeti la HabariLEO Oktoba 27, 2020, ilisema kuwa katika kipindi cha miaka mitano ya uongozi wa Rais Magufuli, serikali ilifanikiwa kuboresha miundombinu ya barabara, madaraja, vivuko na viwanja vya ndege.

Wizara ilisema kuwa katika kipindi hicho, barabara za urefu wa kilometa 2,624.27, madaraja 10 na ukarabati wa barabara za urefu wa kilometa 404.7 katika mikoa mbalimbali nchini, ulikamilika.

Pia katika miaka hiyo mitano ya kwanza ya Serikali ya Awamu ya Tano, zaidi ya kilometa 82.6 za barabara za kupunguza msongamano katika miji zilikamilika kujengwa kwa kiwango cha lami, lakini pia barabara za urefu wa kilometa 1,298.44 na madaraja saba ujenzi wake ulikuwa unaendelea na ulitarajiwa kukamilika ndani ya miaka mitatu baadaye.

Kuhusu miundombinu ya madaraja, Serikali ya Awamu ya Tano ilianza ujenzi wa madaraja ya Kigongo-Busisi la Mwanza, Ruhuhu lililopo Ruvuma, Tanzanite jijini Dar es Salaam, Wami mkoani Pwani, Kitengule mkoani Kagera, Msingi lililopo Singida na la Gerezani Dar es Salaam.

BARABARA ZA JUU

Ili kuondoa au kupunguza tatizo la foleni Dar es Salaam, Serikali ya Magufuli ilitekeleza ujenzi wa Daraja la Juu la Mfugale la Tazara, Dar es Salaam kwa gharama ya Sh bilioni 100.

Ilijenga pia barabara za juu Ubungo zilizopewa jina la John Kijazi kwa gharama ya Sh bilioni 240 pamoja na kuanza upanuzi wa njia nane wa Barabara ya Morogoro kuanzia Kimara-Stop Over hadi Kibaha mkoani Pwani ya urefu wa kilometa 19.2 kwa gharama ya Sh bilioni 141.5. Barabara ya Bagamoyo eneo la Mwenge-Morocco nayo.

Daraja la Tanzanite

ilipanuliwa wakati wake.

USAFIRI WA ANGA

Kwa kuwa dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano ilikuwa kuhakikisha maisha ya Watanzania yanaboreka kwa kuwajengea miundombinu wezeshi ikiwemo ya usafiri na usafirishaji, hivyo ikajikita pia katika upanuzi na ukarabati wa viwanja vya ndege mbalimbali nchini kikiwemo cha Mtwara, Songea na Iringa.

ATCL

Serikali ya Awamu ya Tano pia imeifufua Kampuni ya Ndege nchini (ATCL) kwa kununua ndege mpya ikiwemo Boeing 787-8 Dreamliner moja yenye uwezo wa kubeba abiria 262, Airbus A220-300 mbili zenye uwezo wa kubeba abiria 130 kila moja na Bombardier Das 8 Q400 na kwa kuwa lengo la serikali ilikuwa kununua ndege mpya 11, ndege nyingine zilizobaki, zilinunuliwa na Serikali ya Rais Samia.

MAJI

Miongoni mwa mambo ambayo Rais Magufuli aliyashughulikia kwa jitihada kubwa ni upatikanaji wa maji safi na salama kwa Watanzania katika maeneo mbalimbali nchini.

Wakati wake, Rais Magufuli aliwahi kusema serikali yake ilikuwa inatekeleza miradi 1,400 ya maji nchi nzima ukiwemo mradi mkubwa wa kutoa maji Ziwa Victoria jijini Mwanza kwenda Shinyanga-Nzega-Tabora hadi Igunga ambao pia utatoka Tabora-Itigi-Manyoni umbali wa kilometa 220 na kisha kufika Dodoma kilometa 127 pamoja na mradi wa Sh bilioni 520 mkoani Arusha na miradi mingine mingi kila mahali. Pia mradi wa Kisarawe, Pwani aliuzindua mwenyewe.

 

Muonekano mpya wa Ikulu ya Chamwino, Dodoma.

Aidha, Wakazi wa Mbezi wilayani Ubungo, Dar es Salaam hawatamsahau Magufuli kwa hili. Ni katika kipindi chake maji yaliwafikia kwa wingi saa 24 kila siku kwa wiki.

Miradi hiyo ya maji aliyoianzisha, inaendelea kutekelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita kote nchini.

ELIMU BURE, MIKOPO ELIMU JUU

Moja ya mambo ambayo Watanzania wataendelea kumuenzi Rais Magufuli ni uamuzi wake wa kuanzisha mfumo wa elimu bure kuanzia shule za msingi hadi sekondari kidato cha nne ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya CCM (2015-2020).

Uamuzi huo wa Magufuli ulitoa fursa kwa watoto wengi wa Kitanzania kupata elimu ya msingi na sekondari kwa kuwa ada na michango mingi ilikuwa kikwazo kwa wengi wao.

Kipindi cha miaka mitano ya uongozi wake, serikali ilitumia Sh trilioni 1.09 kwa ajili ya kutoa elimu bure kwa shule ya msingi hadi kidato cha nne kote nchini na ilitumia Sh trilioni 2.28 kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu.

AFYA

Ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya katika maeneo yao, Serikali ya Magufuli ilijenga jumla ya hospitali za rufaa 3, hospitali 10 za rufaa za mikoa, 99 za wilaya, vituo vya afya 487, zahanati 1,198 pamoja na kuongeza bajeti ya dawa kutoka Sh bilioni 31 mwaka 2015 hadi kufikia Sh bilioni 270.

WAMACHINGA/MAMALISHE

Ni katika kipindi chake, Magufuli alisisitiza wafanyabiashara wadogo (wamachinga) wasiondolewe kimabavu na mgambo bali kila mkoa utafute maeneo mazuri yenye miundombinu stahili ndio wahamishiwe huko. Hatua hii pia iliwahusu mama na baba lishe. Kazi hii ya kuwajengea maneeo inaendelezwa kwa sasa.

ATCL

MASOKO/STENDI ZA MABASI

Chini ya uongozi wake, vituo vikubwa vya mabasi (stendi) vilijengwa katika mikoa mbalimbali ikiwemo Dodoma (Nanenane), Mwanza na Kituo Kikuu cha Mabasi cha Mbezi Louis kilichopewa jina lake.

Ndio maana Watanzania walio wengi wataendelea kumkumbuka Rais Magufuli ambao wengi walipenda kumuita JPM, jembe, jiwe, mwamba na kiongozi wa wanyonge. Endelea kupumzika JPM huku kazi ya ujenzi wa nchi inaendelea.

Habari Zifananazo

Back to top button