Esperance vs Mamelodi, Ahly vs Mazembe Nusu Fainali

LUANDA, Angola: KUNGURU wa Lubumbashi, TP Mazembe wakiwa nyumbani watakabiliana na Al Ahly ya Misri, Aprili 19 mwaka huu katika hatua ya Nusu Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika (CAFCL).

Mazembe, wametinga hatua hiyo kibabe kwa ushindi wa mabao 1-2 ugenini dhidi ya Atletico ya Angola katika Uwanja wa Novemba 11, kufuatia mchezo wa kwanza jijini Lubumbashi kutoka suluhu tasa.

Kabla ya mchezo huo, Atletico haikuwahi kuruhusu bao lolote katika michuano ya CAFL inayoendelea.

Upande mwingine Esperance ya Tunisia, mabingwa mara tatu wa CAFCL watakabiliana na mabingwa mara moja wa michuano hiyo, Mamelodi Sundowns katika hatua ya Nusu Fainali, Aprili 19, 2024 nchini Tunisia.

Esperance imefuzu hatua hiyo, kwa changamoto ya mikwaju ya penalti (4-2) dhidi ya Asec Mimosas, Uwanja wa Félix Houphouët-Boigny nchini Ivory Coast baada ya matokeo ya jumla ndani ya dakika 180 kuwa 0-0.

Baada ya michezo ya mkondo wa kwanza Aprili 19, mechi za marudiano zitachezwa Aprili 26, 2024.

Washindi katika michezo hiyo watavaana katika hatua ya Fainali kwa michezo ya nyumbani na ugenini, kuanzia Mei 19 na mkondo wa pili Mei 26, 2024.

Habari Zifananazo

Back to top button