‘EU imepotoshwa bomba la mafuta EAC’

Kanisa Katoliki lapongeza ujenzi bomba la mafuta

JUMUIYA ya Watoa Huduma katika Sekta ya Mafuta na Gesi Tanzania (ATOGS), imesema Bunge la Umoja wa Ulaya (EU) limepewa taarifa za uongo na upotoshaji wa makusudi kuhusu ulinzi wa mazingira na haki za binadamu katika utekelezaji wa Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP).

Kutokana na hali hiyo, wadau wa EACOP Tanzania na Uganda wamesema hatua hiyo ni vita inayolenga kudhoofisha nguvu za kiuchumi katika nchi za Afrika na kuzifanya ziendelee kuwa tegemezi.

Wabunge nchini Uganda wakiongozwa na Naibu Spika wa Bunge, Thomas Tayebwa, wamelaani hoja na azimio la Bunge la Umoja wa Ulaya (EU) wakisema zinalenga ubaguzi wa rangi na kuhujumu maendeleo ya kiuchumi.

Advertisement

Wiki iliyopita, Bunge la EU lilipigia kura azimio la kusimamisha ujenzi wa EACOP kwa madai ya ukiukwaji wa haki za binadamu na athari za kimazingira katika mradi huo unaotekelezwa Uganda na Tanzania.

Katika mazungumzo na HabariLEO Afrika Mashariki jana, Mwenyekiti wa Bodi ya ATOGS, Abdulsamad Abdulrahim alisema ATOGS inaamini hoja iliyofikishwa katika Bunge hilo kuhusu mradi huo, inatokana na taarifa za upotoshaji wa makusudi wa mambo muhimu kuhusu ulinzi wa mazingira na haki za binadamu.

Abdulrahim alisema kabla ya kutazama nchi nyingine kama Uganda ambayo mradi wake hauna athari katika mazingira wala haki za binadamu, EU inapaswa kujitazama kwa kuwa katika miezi ya karibuni, nchi nyingi wanachama wake zimeendelea kuchunguza, kuendeleza na kuongeza uzalishaji na matumizi ya nishati ya mafuta.

“Mradi huu unalenga kuhakikisha mafuta hayo yanasaidia kuleta ukuaji wa uchumi wa kijamii na kuleta mabadiliko nchini Uganda na Tanzania. Mradi pia umepitia Tathmini ya Athari ya Kijamii ya Kimazingira (ESIA) iliyofanywa kwa misingi ya kampuni za Magharibi, kwa viwango vya IFC na mbinu bora za kimataifa pamoja na idadi ya tafiti za kimsingi za baioanuwai na baiolojia,” alisema.

Kwa nyakati tofauti, Waziri wa Nishati wa Tanzania, January Makamba na Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Dk Samuel Gwamaka wamenukuliwa wakisema mradi huo ni salama na hautakuwa na athari zozote mbaya kwa mazingira wala haki za binadamu katika mchakato wote wa utekelezaji wake kwani mambo hayo yamezingatiwa.

Gwamaka alisema: “Baraza limehakikisha kwamba mradi huu wa bomba la mafuta ghafi Afrika Mashariki umezingatia masuala yote ya hifadhi ya mazingira kabla na wakati wa utekelezaji wake.”

Naibu Spika wa Uganda, Thomas Tayebwa, alisema: “Hoja hii inalenga kufifisha maendeleo ya mafuta na gesi ya Uganda na kwa kuongeza, ukuaji wa uchumi wa kijamii na maendeleo ya nchi …. azimio hilo linawakilisha kiwango cha juu cha ukoloni mamboleo na ubeberu dhidi ya uhuru wa Uganda na Tanzania.”

 

 

 

 

 

1 comments

Comments are closed.