EU kuipatia Tanzania tril 2/- za miradi

Balozi waTanzania nchini Ubelgiji, Luxembourg na Umoja wa Ulaya (EU), Jestas Nyamanga

UMOJA wa Nchi za Ulaya (EU) umeahidi kutoa Sh trilioni mbili za msaada kwa Serikali ya Tanzania, kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ikiwamo kukuza uchumi wa buluu.

Balozi waTanzania nchini Ubelgiji, Luxembourg na Umoja wa Ulaya (EU), Jestas Nyamanga alisema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari kwa njia ya mtandao wa zoom.

Nyamanga alisema Tanzania imekubaliana fedha hizo zitumike kwenye sekta ya uchumi wa buluu ambayo ndio ajenda ya sasa nchi na umoja huo tayari umekubali kutoa Euro milioni 140 kwa ajili hiyo.

Advertisement

“Kati ya Euro hizo 140 tumekubaliana Euro 130 zitawekwa kwenye benki kama guarantee, kwa sababu benki zetu ukiwaambia unataka kukopa kwa ajili ya kuwekeza kwenye marine park na fisheries ni ngumu sana kukupa hiyo guarantee na mikopo,” alisema.

Balozi Nyamanga alisema kutokana na hali hiyo waliona fedha hizo kutoka EU ziwekwe kwenye benki ili Watanzania wakazikope kutoka benki na kuwekeza kwenye maeneo hayo.

Alihimiza benki za Tanzania kuona hiyo kama fursa na kuchangia fedha hizo ili ziwekwe kwenye benki zao kwa ajili ya kutoa mikopo.

Balozi Nyamanga alisema katika fedha hizo pia zitatumika kidogo kwa ajili ya kutengeneza sera kwa upande wa bara na kanuni lakini Euro milioni 90 zitakuwa ni kwa ajili ya wajasiriamali wanaotaka kuwekeza kwenye sekta hiyo ya uchumi wa buluu.

“Wale wanaotaka kuwekeza kwenye uvuvi, usafiri wa majini, fukwe na utalii anzeni kuandaa proposal nzuri mkope na kuwekeza kwenye sekta hii ya uchumi wa buluu,” alisema.

Alihadharisha kuwa fedha hizo hazitakuwa na zuio kwa matumizi ya Tanzania pekee bali zinaweza kuchukuliwa na mtu kutoka nchi yeyote anayetaka kuwekeza ndani ya nchi.

Balozi huyo alisema pia wamekubaliana katika fedha hizo EU itatoa Euro milioni 75 kwa ajili ya kutekeleza mradi wa kuboresha mazingira na kufanya miji ya kijani utakaotekelezwa katika miji mitatu ambayo ni Mwanza, Tanga na Pemba.

Alisema taratibu za utekelezaji wa mradi huo zinaendelea na halmashauri na manispaa zilizopo katika miji husika ziandae mipango, mapendekezo na mikakati mizuri itakayoonesha namna watakavyozitumia fedha hizo kubadilisha mwonekano wa miji hiyo.

Aidha, alisema pia kutakuwa na Euro milioni 35 kwa ajili ya uboreshaji wa mifumo ya kidijiti na kubadilisha mifumo ya teknolojia ya habari. Pia, kutakuwa na Euro milioni 70 kwa ajili ya kusaidia masuala ya jinsia.

Balozi alisema umoja huo pia umeanzisha mpango unaoitwa Global Gateway Investment Parkage ambao kwa nchi za Afrika umetengewa Euro bilioni 150.

Alisema upatikanaji wa fedha hizo hautegemei mgawo bali unategemea namna nchi ilivyotengeneza mradi wake wa uwekezaji.

Balozi Nyamanga alisema fedha hizo zitatumika kwa ajili ya kuweka dhamana ya benki na kukopesha wawekezaji wanaotaka kuwekeza maeneo mbalimbali ambapo kwa Tanzania fedha hizo zimeelekezwa katika eneo la uchumi wa buluu.

“Sasa naomba Watanzania wazichangamkie fedha hizi kwa kuandaa miradi mikubwa ambayo itagusa eneo hilo la uchumi wa buluu,” alisema.

Alisema Afrika pia imeandaa korido 11 zinazogusa eneo la miundombinu na Tanzania imepewa korido mbili ambazo mradi wowote wa miundombinu utakaozigusa, utanufaika na fedha hizo Euro bilioni 150. Korido hizo ni Dar es Salaam, Nairobi na Addis Ababa na Mbeya na Kasama, Zambia.

Balozi Nyamanga alisema kupitia Jumuiya ya Afrika Caribbean na Pacific (OSPS) ambayo Tanzania ni mwanachama, nchi imechaguliwa kuwa mwenyekiti kuanzia mwaka huu hadi mwaka 2024 katika masuala ya uvuvi na kilimo. Jumuiya hiyo ina jumla ya wanachama 79.

 

 

 

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *