EWURA yavifungia vituo viwili vya mafuta

DAR ES SALAAM: MAMLAKA ya Udhibiti wa huduma za Nishati na maji (EWURA) imevifungia vituo viwili vya Uuzaji mafuta kwa muda wa miezi sita.

Vituo hivyo ni Gapco Tanzania Limited Moshi Service Station, chenye Leseni Na PRL-2023-104 na Anwar Saleh Bakhamis T/A Serious Oil Petrol Station cheny Leseni Na PRL-2019-228.

Akizungumza na waaandishi wa habari  Dar es salaam, Meneja Uhusiano na Mawasiliano, EWURA, Taitus Kaguo amesema hatua hiyo imechukuliwa kutokana na baadhi ya wamiliki wa vituo vya mafuta kuficha mafuta kwa makusudi wakisubiri ongezeko la bei za mafuta.

“Kwa mujibu wa sheria ya Petroli, Sura Na. 392, Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imepewa jukumu la kuhakikisha upatikanaji wa mafuta wakati wote na katika maeneo yote nchini.”- amesema Kaguo.

“Kuanzia mwezi wa Julai kumekuwepo na matukio kwa baadhi ya maeneo hasa pembezoni mwa nchi kukosa mafuta hasa kipindi bei zinapoelekea kubadilishwa na kusababisha kuwa na usumbufu mkubwa kwa wananchi” alisisitiza Kaguo.

Kaguo amesema hadi sasa EWURA imevifungia vituo 11 kwa muda wa miezi sita kwa makosa ya kuhodhi mafuta kinyume na sheria na vingine bado uchunguzi unaendelea.

EWURA inatoa onyo kwa wamiliki wa vituo vya mafuta kuacha mara moja tabia ya kuhodhi na kuficha mafuta kwa sababu hatua kali zitachukuliwa kwa wanaoficha mafuta ikiwemo kuwafutia leseni zao za biashara.

Habari Zifananazo

Back to top button