MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imesema nchi ina mafuta ya kutosha katika ghala zake za kuhifadhia mafuta na mpaka kufikia Julai 14, 2023 mafuta ya petroli yaliyokuwepo nchini ni zaidi ya lita milioni 169.85
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na mamkala hiyo siku ya Jana, katika kipindi hicho nchi ilikuwa na mafuta lita milioni 209.64 za dizeli na lita milioni 34.58 za mafuta ya ndege hivyo kufanya nchi kuwa mafuta ya kutosha.
Mamlaka hiyo imelazimika kutoa taarifa baada ya kupokea tarifa ya uwepo wa baadhi ya makampuni ya mafuta kuhodhi mafuta kwaajili ya maslahi binafsi ya kibiashara ikiwemo kusubiri mabadiliko ya bei huku kampuni nyingine zinasemekana kupakia mafuta kutoka kwenye maghala pasipo kuyauza na nyingine kukataa kuuza mafuta kwa wamiliki wa vituo wasio kuwa na ubia au mikataba nao.
“Kutokana na hayo EWURA imepata taarifa ya kuchelewa kufikishwa kwa mafuta katika baadhi ya maeneo ya pembezoni mwa nchi na miji,” taarifa ya EWURA ilisema.
Aidha, mamlaka hiyo imezionyo kampuni zote za mafuta zinazohodhi mafuta na kuzitaka kuacha mara moja ikisema ni kinyume cha sheria na kanuni zinazosimamia biashara ya mafuta na petroli nchini.