Faida uwekezaji mpya Tanga Cement zatajwa

WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba amewahakikishia Watanzania kuwa uwekezaji mpya wa zaidi ya dola za kimarekani milioni 400 utakaofanywa na kiwanda cha Saruji cha Twiga kwenye kiwanda cha Saruji Tanga, utaongeza uzalishaji wa saruji, kukuza ajira na mapato ya serikali kupitia kodi mbalimbali.

Dk Nchemba ametoa kauli hiyo leo, Mei 8, 2023 jijini Dodoma walipokutana na kufanya mazungumzo na uongozi wa kiwanda cha Tanga Cement pamoja Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Ashatu Kijaji.

Alisema kiwanda hicho kina mchango mkubwa wa kukuza ajira, kutoa kodi serikalini lakini kikubwa ni kuongezeka kwa uzalishaji wa saruji kunakotarajiwa, ambako kutawafanya wananchi wapate saruji kwa bei nafuu na kujenga makazi bora.

“Uzalishaji ukiwa mkubwa, tuna uhakika wananchi watapata simenti kwa bei nafuu,” alisema Waziri Nchemba.
Aliishauri Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara kuharakisha uwekezaji huo ili ukamilike kama ilivyopangwa.

Kwa upande wake Waziri Ashatu alisema kuwa kiwanda cha Saruji cha Tanga kupata mwekezaji mpya lilikuwa jambo lisilokwepeka kutokana kiwanda hicho kupata hasara kwenye mizania yake ya biashara kwa miaka mitano mfululizo na hivyo kuweka rehani zaidi ya ajira za wafanyakazi 3,000 wa kiwanda hicho pamoja na mapato ya serikali.

Akifafanua alisema mtaji huo wa dola za Marekani milioni 400 ambazo ni sawa na zaidi ya shilingi bilioni 930, utakifanya kiwanda hicho kuzalisha saruji kwa wingi itakayokidhi soko la ndani, Afrika Mashariki, na eneo huru la biashara la Afrika kwa ujumla.

Habari Zifananazo

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x