Fainali za BSS kufanyika Feb. 4
FAINALI za Bongo Star Search (BSS), zinatarajia kufanyika Februari 4, mwaka huu ukumbi wa The Super Dome Masaki jijini Dar es Salaam.
Mshindi wa kwanza wa shindano hilo anatarajiwa kuzawadiwa Sh Mil 20, mshindi wa pili Sh Mil 3 na wa tatu Sh Mil 1.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Benchmark, inayoandaa shindano hilo, Rita Paulsen, amesema msimu huu umekuwa wa tofauti na misimu yote kwa kuwa wamechukuwa washiriki 10 bora wa miaka yote.
“Wamewekwa pamoja washindi waliofika 10 bora na kutengeneza mastaa wapya kwenye msimu huu wa 13, kwa malengo ya kuwapatia mashabiki wa kipindi chetu ladha mpya tofauti na vipindi vingine.
“Kuwapatia wasanii wachanga fursa ya kuonekana zaidi na jamii yetu, kuwawezesha kuwa mastaa kwa nyimbo zao wenyewe hadi sasa waliofika 8 bora wamepata nafasi ya kurekodi na kufanya video za nyimbo zao wenyewe mpya,” amesema.
Aliwataja majaji walioshiriki kuchagua wasanii waliofika fainali ni Rayvany, Shilole, Fid Q, Nandy, Barnaba pamoja na Adam Mchomvu.