Fainali za Ulaya 2024 zaanza leo

Steve Clarke

UJERUMANI – KOCHA Mkuu wa Scotland, Steve Clarke amesisitiza timu yake itaikabili Ujerumani kwa heshima kwenye mchezo wa ufunguzi wa michuano ya Kombe la Mataifa ya Ulaya leo.

Mchezo huo utapigwa katika Uwanja wa Allianz Arena, Munich leo usiku ambapo Scotland imedhamiria kuvuka hatua ya makundi ya michuano hiyo.

Scotland imefuzu mfululizo michuano ya Ulaya lakini ndio mashindano yao ya kwanza tangu fainali za Kombe la Dunia zilizofanyika Ufaransa mwaka 1998.

Advertisement

SOMA: BMT yamtia kitanzi Shomari Kimbau

“Tunajua ni mechi kubwa, kwetu sisi ni mechi ya ufunguzi kwenye kundi lenye timu nne, mechi tatu na tunajua tunatakiwa kusonga mbele na hilo ndilo tunaloliwekea mkazo,” alisema.

Ujerumani iko mbele kwa nafasi 23 zaidi kwenye viwango vya ubora wa Fifa, lakini Clarke bado ana imani timu yake itasonga mbele.

“Tuna imani tunaweza kupata matokeo kila mara tunapoingia uwanjani, kama tunakosa imani hiyo hakuna sababu ya kuingia uwanjani kucheza,” alisema kocha huyo wa zamani wa Kilmarnock.

“Tumejiandaa vizuri, tuko tayari na tuna imani tunaweza kuonesha hilo. Nafikiri wote tunapaswa kujivunia kuwa hapa. Ni muda mrefu umepita tangu mwaka 1998 tuliposafiri kwenda nje kwa ajili ya mashindano kama haya,” alisema.