Familia ya Mkono yajipanga kuupokea mwili

FAMILIA ya mwanasiasa na wakili maarufu nchini, Nimrod Mkono imesema imekamilisha taratibu za kurejesha mwili wa kiongozi huyo kwa asilimia 99.

Mdogo wa marehemu, Zadock Mkono amesema wanamsubiri binti wa marehemu Mkono, Leah Mkono afike kutoka Marekani ili asaidie kukamilisha maandalizi ya kuupokea mwili.

Zadock alilieleza HabariLEO kuwa binti huyo atakapofika ataungana na kamati inayoratibu taratibu za kuurejesha mwili wa marehemu Mkono.

“Bado taratibu za kuleta mwili zinaendelea lakini uhakika wa kuuleta nchini ni asilimia 99.

“Ni kama zimekamilika, kwa hiyo kwa sasa tunangojea binti yake aje nchini kutoka Marekani kusaidia maandalizi ya kupokea mwili,” alisema.

Zadock alisema kwa mujibu wa taarifa walizopewa binti huyo anatarajiwa kuwasili nchini ndani ya wiki mbili au tatu tangu siku kilipotokea kifo cha Mkono hivyo bado wako ndani ya muda wa matarajio hadi sasa.

Mkono aliaga dunia Aprili 18, mwaka huu jijini Florida nchini Marekani alipokwenda kutibiwa.

Zadock alisema mwishoni mwa wiki hii, familia itakuwa katika wakati mzuri kutaja tarehe ya kuwasili mwili wa mpendwa wao baada ya binti huyo kuwasili na kuweka taratibu vizuri kwa kushirikiana na kamati atakayoikuta.

Mkono alikuwa ni wakili na mwanasiasa nguli aliyewahi kushikilia nafasi ya ubunge katika Jimbo la Musoma Vijijini mkoani Mara mwaka 2000 hadi 2015 na baadaye jimbo la Butiama mwaka 2015 hadi 2020.

Akiwa Mbunge alisaidia maendeleo katika Jimbo la Butiama ikiwa ni pamoja na kushiriki kuanzishwa Chuo Kikuu cha Kilimo na Teknolojia cha Mwalimu Nyerere. Mkono ameacha mjane na watoto wanne.

Habari Zifananazo

Back to top button