Familia yagoma kuzika aliyeua mama wa kambo

FAMILIA ya Jackson Msafiri (25) aliyeuawa na wananchi baada ya kumuua kwa mapanga mke wa baba yake (mama wa kambo), Elinata Elias (27) imegoma kuzika mwili wa kijana huyo.

Tukio la mauaji ya watu hao lilitokea Februari 16 mwaka huu saa 2:30 usiku nyumbani kwa marehemu Mtaa wa Kilimahewa, Kata ya Ludete Mji Mdogo wa Katoro wilayani Geita.

Msemaji wa familia, Galebo Galebo aliwaeleza hayo waandishi wa habari mara baada ya ibada ya mazishi ya mwili wa Elinata alyeuawa huku akiwa mjamzito.

Galebo alisema hadi sasa, miili ya Jackson na rafiki yake walioshiriki mauaji ya Elinata bado ipo mochwari na familia haina mpango wa kuichukua miili na wameliachia Jeshi la Polisi.

“Wale kweli ni ndugu zetu, lakini wapo chini ya mamlaka ya Polisi, kwa hatua ambazo tumeshachukua, tumeachia taratibu za Jeshi la Polisi, familia haiko tayari kuzika,” alisema na kuongeza:

“Nawashauri vijana waache tamaa, wajishughulishe na kazi, endapo kuna tatizo linamsumbua kijana ni vyema amuone mzazi wake wakae chini waongee.”

Mtendaji wa Kata ya Ludete, Martin Matiba aliwaomba wananchi watoe taarifa mapema wanapokutana na migogoro ya kifamilia inayotishia usalama wao ili mamlaka zichukue hatua haraka.

“Kwa tukio hili nadhani kila mmoja aliyepo hapa ameumizwa na kitendo hiki, kwa hiyo nawaombeni sana tuimarishe malezi kwa watoto wetu, tuimarishe malezi kwenye familia.

“Tukio linalosababishwa na mtoto ndani ya familia ni kitendo cha ajabu sana, ni kitendo cha aibu, lakini ndio imeshatokea, aliyeua naye akauawa,” alisema.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Geita, Ofisa Tarafa ya Katoro, Kassim Ramadhan alisema kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya imejipanga kuwashughulikia vijana wahalifu wanaotishia usalama katika jamii.

Kassim aliwataka wenyeviti na watendaji wa mtaa, vitongoji na vijiji waweke mikakati kushirikiana na wananchi ili kuwafichua vijana wanaotishia usalama ndani ya jamii.

Habari Zifananazo

Back to top button