Familia yaomba mume aliyeua mkewe asakwe

NDUGU na majirani wa mwanamke aliyedaiwa kuuawa na mumewe kwa kuchomwa na kitu chenye ncha kali mwilini katika Mtaa wa Lukirini, mjini Geita wameiomba serikali kuchunguza kwa undani na kumpata mtuhumiwa.

Akizungumza jana baada ya shughuli ya kuaga mwili wa marehemu Amina Hassan (34) na kwenda Dodoma kwa maziko, mjomba wa marehemu, Bakari Hamza alisema wanafamilia wanatamani kuona haki inatendeka.

“Huyu bwana aliyefanya hili tukio, serikali ya hapa Geita naiomba sana ifuatilie huyu mtu, ili walau aweze kuonekana kwa haraka sana, ili tuweze kujua ni nini chanzo, kwa sababu sisi ni watu lakini maamuzi aliyochukua si sahihi,” alisema.

Advertisement

Mwenyekiti wa Mtaa wa Mkoani (Lukirini), Salvatory Paulo alieleza chanzo cha mauaji hayo kuwa  kimeonekana ni ugomvi wa wanafamilia hao jambo ambalo linawakumbusha wanandoa wote kufanya usuluhishi mapema wa migogoro inapotokea.

“Kwa hiyo naomba tujifunze kupitia tukio hili. Ndoa si lazima, ndoa ikileta shida ni vyema muachane kuliko mmoja abaki amekufa, mwingine anakimbia, ni nafuu ndoa ife ili wote mbakie salama, watu wapo wameachika na wanaendelea na maisha,” alisema Paulo.

Diwani wa Kata ya Kalangalala mjini Geita, Pudence Temba aliwaomba wanaume kuwa wawazi wanapokutana na changamoto ndani ya familia na kuwashirikisha viongozi wao wa mitaa na kata ili kuepuka kuchukua uamuzi wa kikatili.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Ally Kitumbu alithibitisha kuwa Amina aliuawa na kumtaja mtuhumiwa wa tukio hilo kuwa ni mumewe, Mashaka Jeremia. Tukio hilo ni la Agosti 30, mwaka huu.