Familia zahaha kutoweka kwa ndugu

Familia zahaha kutoweka kwa ndugu

NDUGU wa familia tatu za watu waliotoweka katika mazingira tatanishi, wanaomba juhudi zifanyike kuokoa maisha ya jamaa zao na kuwarejesha nyumbani.

Martin Mungia, Vincent Owuor na James Muthee, walitoweka kwa tarehe tofauti kati ya Juni 30 na Septemba 15, mwaka huu jijini Nairobi.

Juni 30 akiwa nyumbani kwao maeneo ya Roysambu, Mungia aliondoka akisema alikuwa akielekea kukutana na rafiki yake huko Ruiru, lakini hakurudi.

Advertisement

Mama wa Mungia, Mary Mungai alisema: “Rafiki yake ambaye alisema angekutana naye alinipigia simu akiuliza aliko Mungia na nilipoamua kumpigia pia simu yake kujua alipo, ilikuwa imezimwa.”

Kijana huyo alishindwa kufika usiku huo hali iliyowalazimu kuripoti kisa hicho katika Kituo cha Polisi cha Kasarani na aliwekwa chini ya OB namba 111/30/6/2022.

Kwa mujibu wa mama huyo, mwanaye aliyetoweka alikuwa mwandishi wa mtandaoni na polisi bado hawajapata kidokezo chochote kuhusu kutoweka kwa Mungai.

“Sijui kama mwanangu yu hai au amekufa…,” alisema mama huyo.

Kuhusu Vincent Owuor, yeye alitoweka Septemba 13 katika kile kinachodhaniwa na familia yake kuwa ni kutekwa nyara.

Siku alipotoweka ofisini kwake Kilimani, inaripotiwa kuwa wanawake wawili waliovalia hijabu na wanaume watatu wakiwa na Prado nyeupe walimchukua ofisini kwake wakijitambulisha kuwa ni askari polisi.

Tukio hilo limeripotiwa katika Kituo cha Polisi cha Kilimani chini ya OB namba /68/14/09.

Mkewe Owuor Risper alisema kwa sasa ameachwa na watoto wawili wa kuwatunza huku msako wa kumtafuta mume ukiendelea.

“Wanaendelea kuniuliza baba yao atarudi lini na mimi pia ninashangaa, kwa nini mtu anataka kumdhuru mtu mwenye amani?” Risper alijiuliza.

“Inashangaza kwamba polisi hawajasema lolote kuhusu kesi hiyo, ingawa barabara zote za Milimani zina kamera za CCTV,” alisema.

Katika tukio lingine, inadaiwa kuwa ni miezi mitatu sasa tangu James Muthee kutoweka ikidaiwa kuwa, alikamatwa eneo la Kamakis na watu sita waliojitambulisha kuwa maofisa wa polisi.

Siku hiyo, alisema kwamba wavamizi walizuia gari la Muthee, wakamtoa nje na kumfunga kwenye gari lao na kusogea mbali.

Baba wa Muthee, John Mwangi alisema: “Inasikitisha sana kwamba baadhi ya watu mahali fulani wameamua kumficha. Sijui hata kama wamemuua na nataka hata kufikiria hivyo! Ninachotaka ni kuambiwa aliko mwanangu…”

Familia ya Muthee ilisema iliripoti kisa hicho kwa mara ya kwanza katika Kituo cha Polisi cha Juja ambapo walisema watachunguza kisa hicho hadi sasa.