MARA kadhaa tumesikia fulani amekufa kutokana na moyo kusimama ghafla. Au alikuwa anafanya jambo fulani ghafla akadondoka na kufa au mchezaji anacheza uwanjani ghafla anadondoka anakufa.
Hayo yote ni matatizo yanayojulikana kitaalamu kama moyo kusimama ghafla (cardiac arrest).
Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), ametaja visababishi vya mtu kupata tatizo la moyo kusimama ghafla huku pia akitoa elimu ya jinsi ya kumsaidia mtu huyo ndani ya dakika tatu tangu kutokea kwa tatizo na mgonjwa akazinduka.
HabariLEO ilifanya mahojiano maalumu na daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kutoka taasisi ya JKCI, Khuzeima Khanbhai kuhusu tatizo la moyo kusimama ghafla na visababishi vyake na akaeleza kwa upana sababu na jinsi ya kuokoa maisha ya mgonjwa huyo ndani ya dakika chache.
Anasema sababu ya kwanza ya mtu kupata tatizo la moyo kusimama ghafla ni kuwa na matatizo ya mfumo wa umeme wa moyo, mishipa ya damu kuziba, mtindo wa maisha ambao una unywaji wa pombe na uvutaji wa sigara, misuli ya moyo kutanuka.
Akizungumzia tatizo la mfumo wa umeme wa moyo, Dk Khuzeima anasema wagonjwa wenye shida ya mfumo wa umeme wa moyo ama wa kuzaliwa nao au kuupata baadaye wanaweza kukumbwa na tatizo la moyo kusimama ghafla kwa muda, wakati na mahali popote.
“Kama mtu akiwa na tatizo la mfumo wa umeme wa moyo ambao ni ama wa juu au wa chini ikiwa na maana mapigo ya moyo kwenda haraka isivyo kawaida au kwenda taratibu isivyo kawaida, uwezekano wa kupata tatizo la moyo kusimama ni mkubwa,” anabainisha Dk Khuzeima.
Anasema mtu mwenye tatizo la mfumo wa umeme, anaweza kuwa ni wa kuzaliwa nalo kwa maana ya kurithi au kulipata wakati wa kukua kwake na hiyo inaweza kusababisha moyo kusimama ghafla.
Pia, mtu mwenye shida ya mishipa ya damu kuziba kwenye moyo na unywaji wa pombe pamoja na uvutaji wa sigara vinaweza kusababisha mtu akapata tatizo la moyo kusimama ghafla.
“Moyo ukiwa na shida yoyote iwe ya kutanuka kutokana na unywaji wa pombe, mishipa kuziba na mtindo mbaya wa maisha ambao ni pamoja na lishe mbaya na vyakula vya mafuta mengi, unaongeza uwezekano wa moyo kusimama ghafla,” anasema Dk Khuzeima.
Kuhusu dalili za anayepata tatizo hilo, Dk Khuzeima anabainisha kuwa zinatokea muda mfupi kabla ya kukumbwa na tatizo hilo hivyo si rahisi kuona dalili na kuzuia lisitokee lakini upimaji wa afya mara kwa mara unaweza kusaidia kupunguza uwezekano wa kupata maradhi ya moyo yanayochangia moyo kusimama ghafla.
“Moyo kusimama ghafla unawakumba watu wote lakini pia wachezaji wa mpira wakiwa uwanjani, ghafla anadondoka na sio kwamba alikuwa na dalili akazembea la hasha, huwa tatizo linatokea ndani ya muda mfupi baada ya dalili kutokea,” anasema Dk Khuzeima.
Hata hivyo, Dk Khuzema anatoa elimu jinsi ya kuokoa maisha ya mgonjwa kwenye tatizo hilo ndani ya dakika tatu tangu hali hiyo itokee kuwa ni endapo mtu atapata shida hiyo ina maana ataanguka ghafla. Ni vyema kumlaza chali na kuanza kumpa huduma ya kwanza ya kuushtua moyo kwa kumfanyia CPR.
“Huduma ya kwanza ya kuufufua moyo na mapafu (CPR), imeonesha inapofanywa kwa usahihi kwa mgonjwa, unaokoa maisha yake kwa asilimia zaidi ya 95 ndani ya muda sahihi mara tu baada ya mtu kupata tatizo hilo,” anasema Dk Khuzeima.
Anashauri, huduma ya kwanza ya CPR inapaswa kutolewa kuanzia shuleni hadi nyumbani ili watu wengi wafahamu jinsi ya kumsaidia mgonjwa na kuokoa maisha.
Anasema moyo unaposimama ghafla, ina maana damu inakuwa haipelekwi kwenye maeneo yake ikiwemo kwenye ubongo, mapafu na maeneo mengine hivyo mgonjwa anapofanyiwa CPR ambayo ni kumpampu kifuani mgonjwa kwa kutumia mikono unamsaidia kuushtua moyo na damu kutembea hivyo anaweza kupona.
Huduma hiyo ya CPR, inafanywa kwa kupampu kifua cha mgonjwa mara kadhaa na kuacha kusikiliza kama pumzi anavuta, kisha kuendelea tena hadi pale msaada wa dharura utakapofika ikiwa ni gari la kubeba wagonjwa au mtoa huduma ya afya ambaye naye ataendelea kumfanyia huduma ya CPR hadi mapigo ya moyo yaanze kurudi.
Anasema baada ya hapo, mgonjwa anatakiwa awahishwe hospitalini au kwenye huduma ya afya iliyo jirani kwa ajili ya uangalizi zaidi wa tiba.
Utafiti wa madaktari wa Marekani mwaka 2017 unaonesha kuwa kati ya watu 100,000 watu 74 wanapata tatizo la moyo kusimama ghafla nje ya hospitali na kati ya watu saba mmoja anafariki kwa tatizo hilo.
Hata hivyo, anabainisha dalili za kupata tatizo hilo ni pamoja na kizunguzungu, kifua kuuma ghafla, pumzi kubana au kusikia kichefuchefu.
“Dalili hizo hutokea sekunde au dakika chache kabla ya mtu hajapata tatizo la moyo kusimama ghafla na dalili hizo si kwamba zinatolea siku moja au wiki kadhaa, hapana ni kitendo cha muda mfupi kisha tatizo linatokea, hivyo ni vigumu kuzibaini, mara nyingi mgonjwa akifanikiwa kupata msaada, na kupona ndipo anaeleza alivyosikia kabla ya kuanguka ghafla,” anasema Dk Khuzeima.
Anasema elimu ya huduma ya kwanza ni muhimu na mataifa yaliyoendelea inatolewa hadi nyumbani na watu wanaopata matatizo ya kiafya ghafla husaidika kwa kuwa elimu ipo na kusisitiza elimu hiyo ni vizuri ikatolewa kwa Watanzania wote hadi nyumbani ili kuokoa maisha.
Mbali na elimu hiyo, anashauri kuwa mtindo wa maisha wa sasa hasa kwa vijana wa unywaji wa pombe na uvutaji wa sigara unachangia maradhi mbalimbali ya moyo na kusema kuna utafiti waliufanya katika Hospitali ya Taifa Muhimbili Tawi la Mloganzila mwaka 2019/20 ulioonesha vijana wengi wana matatizo ya moyo bila kufahamu hivi sasa.
Katika utafiti huo wa magonjwa ya moyo, ilibainika kuwa vijana wengi hivi sasa wanapata kiharusi (stroke) kuliko wazee na hiyo ni kwa sababu wengi wao wana shinikizo la juu la damu na hawafahamu kama wana tatizo hilo kwa sababu hawana tabia ya kupima afya.
“Ushauri wangu tujitokeze tukisikia kuna kambi za matibabu, tupime tutambue afya zetu ili tujue na kama kuna matatizo tuanze tiba mapema kwa sababu gharama za kutibu ni kubwa kuliko gharama za kuzuia,” anashauri Dk Khuzeima.
Anabainisha kuwa asilimia tano ya Watanzania wana shinikizo la damu na idadi inazidi kuongezeka kutokana na kuongezeka kwa kasi ya unywaji wa pombe kali na uvutaji wa sigara unaofanywa na vijana ambao unachangia ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza kama ya moyo kutanuka na mengine.
“Tuwasaidie vijana, idadi ya vijana wenye maradhi ya moyo inaongezeka, wengi wanakuja moyo umeshapanuka kwa sababu ya kunywa pombe kali, mtu anaanza kunywa pombe mapema, anavuta sigara, tuwasaidie wapunguze na kuacha. Ukiacha kuvuta sigara leo, unaongeza umri wa kuishi kwa miaka mitano mbele,” anasema Dk Khuzeima.
Mbali ya magonjwa ya moyo pia mtu mwenye tatizo la sukari naye yuko hatarini kupata tatizo la moyo kusimama ghafla na kuwa hatua za kuchukua kupunguza uwezekano huo ni kupima afya na kugundua hali ya mwili na viungo vyako kama kuna hatari yoyote hatua zichukuliwe kudhibiti ili kukuondoa kwenye kundi la hatari.
“Lakini kama kwenye familia kuna mtu alishapata tatizo hilo, uwezekano wa mtu mwingine katika familia hiyo kuupata ni mkubwa, kwa sababu kuna masuala ya genetiki ya kurithi, hivyo kucheki afya yako kutasaidia kuokoa maisha yako na kupewa ushauri na madaktari,” anabainisha Dk Khuzeima.
Anasema kwa watu waliofikisha umri wa miaka 40 kupima afya ni jambo muhimu angalau mara moja kwa mwaka na kama katika familia kuna historia ya kuwa na maradhi ya moyo ni vyema wanafamilia wanapofikisha umri wa miaka 35 kupima afya mara kwa mara.
Mbali na hilo mtindo wa maisha wa unene kupita kiasi, ulaji mbaya wa lishe na kula vyakula vya mafuta mengi zinaweza kumletea mtu kupata tatizo la moyo kusimama ghafla na kushauri wananchi wafanye mazoezi angalau saa moja kila siku ili kuuweka mwili vizuri.
Anasema kwa sasa matatizo ya magonjwa ya moyo ni mengi na katika taasisi ya JKCI, wanapokea wagonjwa wenye shida ya mfumo wa umeme na mishipa ya moyo kuziba na sasa tatizo la mfumo wa umeme linaongezeka zaidi kwa vijana hivi sasa.
“Tunapata vijana wana shida ya mfumo wa umeme, tuna mitambo na vipimo vinavyoweza kubaini matatizo hayo kwa sasa pale JKCI na wale tunaowabaini tunawapa tiba kwa kuwawekea vifaa kwenye moyo (pacemaker),” anasema Dk Khuzeima.
Anashauri wananchi wajenge tabia ya kujitokeza kupima afya zao na pia kambi za kitaaluma za tiba zinapotangazwa wananchi wajitokeze kwa wingi ili wapimwe na kugundua matatizo mapema na kulitibu kuliko kuchelewa na kufanya liwe kubwa zaidi.
“Unachobaini tatizo au viashiria vya tatizo unaweza kulidhibiti, lakini ukichelewa tiba ni ghali na utatumia dawa kwa maisha yako yote, na hiyo ndiyo sababu ya magonjwa yasiyoambukiza yanaongezeka na yanaifanya serikali inatumia fedha nyingi, tuyadhibiti kwa sababu yanadhibitika,” anashauri Dk Khuzeima.