WATAALAMU wa afya nchini wametakiwa kufanya tafiti zenye uvumbuzi, ili kuleta mabadiliko ya kimatibabu nchini na duniani kwa ujumla.
Akizungumza katika kongamano la kwanza la shambulio la moyo lililofanyika leo jijini Dar es Salaam, Naibu Waziri wa Afya, Dk Godwin Mollel amesema nchi zilizoendelea hazina nguvu kwa sababu wana rasilimali nyingi, ila nchi hizo zina nguvu kwa sababu wamewekeza kwa watu wenye akili kubwa, ambao wanafanya uvumbuzi.
“ Na nchi hizo kuwekeza kwa watu wenye akili kubwa na hao watu wanakaa chini wanakuja na uvumbuzi na wakavumbua vitu ndani ya nchi yao, ambapo uvumbuzi huo hakuna mtu wa nchi yoyote anayejua,” ameeleza.
Ameongeza;“Sasa swali ni kwamba pamoja na kujadili moyo waongeze ajenda moyo kwenye suala la uvumbuzi, waje na wazo jipya kabisa wakae waangalie tumefikia wapi, serikali ifanye nini.”
Dk Mollel amesema wanataka kusema mbinu hii ya tiba imegunduliwa na Dk Kisenge wa JKCI na mbinu hii ya tiba imegunduliwa na Prof Janabi wa Muhimbili au dawa hii imetengenezwa na kugundulika Tanzania na chanjo iliyogunduliwa Tanzania.
“Tunahitaji kuchangia duniani tunanunua teknolojia na madaktari kutoka sehemu mbalimbali wamekuja kuleta ujuzi ndani ya nchi na watu wetu tumewapeleka nje, wamejifunza ugunduzi ni muhimu sasa,” amesisitiza.
Amebainisha kuwa Rais Samia ametoa Sh billioni 6.1 kwa ajili ya watu kufanya tafiti, lakini wengi wao wanafanya mambo ya kawaida kama kudodosa, halafu wanasema wamefanya utafiti, hivyo wanataka watu wanaofanya vitu vikubwa.
Akizungumza kuhusu mshtuko wa moyo amesema unatokea ghafla, ambapo asilimia 31 ya watu duniani hufariki kwa matatizo ya moyo na nchini ni asilimi 7.6.
Amesema wataalamu hao wamekutana kujadili kwa kina kuhakikisha wanagundulika mapema na kutibiwa mapema, ili wasiweze kufika hali ya kifo.
Amesema wataalamu hao wanawaachia ujuzi na pia wanajifunza kutoka kwa wataalamu wa ndani kwa sababu wanatofautiana kufikiria namna ya kupunguza magonjwa.