Farao aliyepeleka msiba Ghana
WAKATI baadhi ya mataifa kwenye michuano ya AFCON yakiendelea kuumizana, tujikumbushe Farao mmoja wa kuitwa Mohammed Nagy ‘Gedo’ aliyepeleka msiba usiokuwa na matanga nchini Ghana mwaka 2010.
Baada ya maziko yaliyochukuwa takribani dakika 90 katika uwanja wa Ohene Djan ambao kwa sasa unatambulika uwanja wa ACCRA, wakati shughuli za maziko zikiendelea, kiongozi wa Mafarao, Hassan Shehata aliamua kumsimamisha Mohammed Nagy ‘Gedo’ dakika ya 70 na kwenda kumaliza zoezi hilo.
Gedo alitumia dakika 15 tu kukamilisha zoezi hilo akisaidiana na Mohammed Zidan ambaye alimpa pasi yenye viwango na hakutaka kufanya makosa.
Wakati kikosi cha Hassan Shehata kikiwa na shehena ya wachezaji wa maana kwa wakati ule, akiwemo Ahmed Hassan, Emad Moteab, Hossam Ghaly na wengineo, ila kwenye baadhi ya misiba mingi, Shehata alimtumia Gedo kukamilisha shughuli za maziko.
GEDO vs Nigeria (Makundi)
Ulikuwa mchezo wa kwanza wa makundi AFCON 2010, uliopigwa Januari 12, 2010. Gedo aliingia dakika ya 72 kuchukua nafasi ya mtaalam, Hosny Abd Rabo aliingia Misri akiwa mbele mabao 2-1 wakati huo Nigeria ikifanya jitihada za kutaka kusawazisha.
Dakika ya 82, Gedo alipiga shuti kali nje ya boksi na kumshinda aliyekuwa kipa wa Nigeria, Vincent Enyeama na kufuta matumaini ya Nigeria kutaka kusawazisha.
GEDO vs Msumbuji (Makundi)
Mchezo wa pili Gedo hakufunga bao, ila mchezo wa mwisho wa kundi C, Gedo alinzia nje, wakati mchezo ukiendelea Misri ikiwa mbele kwa bao 1-0 ilionekana kama vile wanataka kusawazisha ikabidi Shehata amuinue Gedo dakika ya 68 na dakika ya 81 Gedo akaweka chuma ya pili.
Mchezo huo uliisha kwa matokeo hayo, na Misri kusonga hatua ya 16 bora. Gedo anaingia akiwa na mabao mawili.
GEDO vs Cameroon (Robo fainali)
Misri iliichapa Cameroon mabao 3-1 katika mchezo wa robo fainali, kwa mara nyingine ‘Gedo’ anaingia na kuweka msumari wa tatu katika ushindi huo. Gedo alifunga bao dakika ya 90.
Katika mchezo huo uliopigwa uwanja wa Ombaka, Cameroon ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya25, na Ahmed Hassan kusawazisha dakika ya 37 kabla ya mchezo huo kwenda dakika 30 za nyongeza.
Gedo aliweka kambani bao la pili dakika ya 90 akitokea benchi, kisha Ahmed Hassan kuweka kamba ya tatu dakika ya 104.
GEDO vs Algeria ( Nusu fainali)
Katika mchezo huo ambao Algeria ilikubali kamba 4-0, mpaka dakika ya 80 mchezo ulikuwa unasomeka 3-0, dakika ya 59 kocha Hassan Shehata alimpa nafasi kwa mara nyingine Gedo akichukuwa nafasi ya Mahmoud Fathalla.
Gedo aliweka chuma ya nne dakika ya 93+ na hivyo Misri kwenda fainali ya michuano ya AFCON mwaka 2010.
GEDO vs Ghana (Fainali)
Ilikuwa mechi ya kiwango sana, yenye kubeba maono ya mataifa hayo, mchezo ulikuwa mgumu sio kawaida, kilichovutia zaidi ni kuona wachezaji wenye hadhi kwa pande zote mbili wakionesha ufundi wa hali ya juu.
Mpaka dakika ya 70 hakuna aliyekuwa amepata bao, na ndio dakika ambayo Farao Gedo aliinuliwa na Shehata kwenda kumaliza kali aliyotumwa.
Dakika ya 85, Gedo akiwa anaongoza mashambulizi na Mohammed Zidan, zilipigwa pasi mbili za haraka kwenye boksi kisha Gedo kufunga bao pekee lililoamua ubingwa kwa Misri.
Michuano hiyo iliisha Gedo akiwa mfungaji bora akiwa na mabao matano. Huyu ndiye Farao wa Misri aliyechukuwa ufungaji bora katika michezo ambayo ametokea bench tu.