SHIRIKA la kimataifa la wanyamapori limesema Kenya imekuwa na ongezeko la asilimia 11 ya idadi ya faru kutoka 1,441 mwaka 2019, hadi 1,605 mwaka jana na hakuna waliopotea kwa ujangili.
Mkurugenzi wa Mfuko wa Kimataifa wa Ustawi wa Wanyama Afrika Mashariki (IFAW, James Isiche amesema miaka nane iliyopita kulikuwa na vitendo vingi vya ujangili vilivyosababisha kupungua kwa faru.
Alisema katika miaka ya karibuni zimechukuliwa hatua mbalimbali za kulinda faru licha ya kuwa janga la ugonjwa wa covid-19 lilisababisha hofu ya kuongezeka kwa ujangili wa wanyamapori.
Alisema, hatua zilizochukuliwa na Shirika la Huduma ya Wanyamapori Kenya (KWS) na washirika kama IFAW zilihakikisha usalama wa wanyama hao walio katika hatari ya kutoweka.
“Tunapongeza wadau wote wa usalama wa wanyamapori na wakala kwa mafanikio haya makubwa katika kupambana na uhalifu wa wanyamapori na kuhakikisha faru wanakuwa salama Kenya.”
“Tuna furaha kwamba idadi ya faru nchini imeongezeka kwa mara ya kwanza, kwa muda mrefu hakukuwa na faru waliokufa kutokana na ujangili,” Isiche alisema.