Fatma Karume akoshwa TSN kutafuta historia yake

MKE wa Rais wa kwanza wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Abeid Karume, Fatma Karume (94) amefurahi waandishi wa Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN) kumtafuta ili kujua historia yake na mambo mengine ya miaka ya nyuma.

Fatma alisema hayo wakati anazungumza na waandishi wa TSN nyumbani kwake Maisara, Zanzibar. Kwa mujibu wa mama huyo, jina lake ni Fatma Gulam Hussein Jamal ila kwa sasa jamii inamfahamu kwa jina la Fatma Karume.

“Kwanza nashukuru kwa kuja kwenu, kunitafuta kwa bidii, kwa dhamira kubwa, kutaka kujua mambo yaliyopita. Kwa hilo, nashukuru sana vijana kwa kuwatafuta wazee ambao bado wapo hai kupata kujua mambo yaliyopita,” alisema.

Akaongeza: “Hili jambo, kwanza limenifurahisha sana la kuja kwenu nyumbani kwangu, nawashukuru na ninawakaribisha, karibuni, mjisikie mko nyumbani.

Vijana mnataka kujua habari za zamani na mnataka kujua asili ya watu namna walivyokutana kwa sababu ninyi mnakutana maskuli (shuleni), sisi wakati huo hatuna skuli, kwa hiyo mlikuwa mnahitaji sana mjue walikutana wapi watu hawa, hasa mimi.

” Fatma anasema alizaliwa Februari 2, 1929 Kaskazini B katika Kijiji cha BumbwiniMisufini Mperani mwisho wa njia wakati huo. Anasema mama yake mzazi alikuwa anaitwa Mwanaisha binti Mbwana Ramadhan na alikuwa mwanamke mzuri aliyependeza.

Fatma alisema Waasia walifika Zanzibar miaka mingi na wengi walizaliwa visiwani humo, hivyo kulikuwa na Wahindi wengi na mama yake upande ni Mswahili na upande ni Mwarabu.

Anasema mama yake alikuwa na kaka zake wakubwa na kaka yake mdogo wa mwisho ambaye alikuwa wakicheza pamoja kwa kuwa watoto wa Kihindi walikuwa wanacheza na watoto wa Kiafrika Bumbwini.

“Mama yangu mkubwa aliolewa mjini hapa na bwana mmoja wa Kiarabu, wakawa wana shughuli za bendi za dansi, huyu Mzee Karume kwa hadithi yake alivyokuwa akinihadithia wakati niko mke wake alipokuwa kijana sana alipenda sana kufanya mambo ya baharini na alitembelea maeneo mengi kama Afrika Kusini, Madagascar, Uingereza lakini India alikaa sana,” anasema Fatma.

Akasema Karume alikuwa kijana mstaarabu na walikutana kwa mara ya kwanza wakati wa sikukuu ya kidini nyumbani kwa mama yake mkubwa.

“Nawaelezeni alivyonipata sasa, yeye (Karume) yuko nje anaongea na baba yangu, nilipotoka ndani, akamuuliza baba yangu, huyu mtoto wa nani? Akamwambia ni mwanangu, ndo ilivyoanzia huku, akamuuliza mbona mtoto wa kihindi huyu? Akamjibu awe Muhindi, awe nani, ila ni mwanangu huyu,” anasema Fatma.

Akasema siku ya pili, baba yake mkubwa ambaye alikuwa mwanamuziki wa dansi aliwachukua yeye na mtoto wa dada yake akawapeleka kwenye ukumbi ambako walikuwa wanapiga dansi na huko alikutana tena na Karume.

Fatma anasema baada ya hapo Karume alikwenda tena kwa wazazi wake kwa lengo la kutaka kumposa. Anasema baba yake mzazi alikuwa Meya wakati huo na alitoa ruhusa kwa binti yake aolewe, na yeye Fatma aliridhia kuolewa kwa kuzingatia sheria ya Kiislamu, hivyo Karume alipeleka posa na ndoa ikafungwa.

“Nilifunga ndoa nikiwa na umri wa miaka 15 mwaka 1944. Basi nimeishi naye, nikakaa naye, nikazaa mtoto wangu wa kwanza wa kike, tukampa jina Asha lakini kwa bahati mbaya alizaliwa akiwa na miezi saba na wakati huo hakukuwa na mashine ya kuhifadhi watoto njiti, alipata baridi na baada ya siku mbili akafariki,” anasema Fatma

. Aliongeza: “Baadaye tukaja tukampata huyu Rais mstaafu (Amani Abeid Karume) na Balozi Ali Karume mpaka tulipofika hapa tulipofika, hiyo ndo historia yangu na mume wangu mzee Karume.

” Kuhusu elimu, Fatma anasema alijiendeleza kielimu akiwa tayari yuko kwenye ndoa kwa kuwa wakati huo hakukuwa na shule na alifanikiwa kusoma takribani madarasa sita. Akasema hadi sasa wajukuu zake wanaendelea kumfundisha, hivyo bado ni mwanafunzi.

Mahojiano haya yataendelea Alhamisi wiki hii.

Habari Zifananazo

5 Comments
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button