DAR ES SALAAM: Tume ya Ushindani nchini (FCC) imesema walaji wanahofu kuhusu matumizi ya akili bandia(mnemba) katika utoaji wa huduma nchini hivyo kuna haja ya kumlinda mlaji ikiwemo uwepo wa kanuni na sheria.
Wadau kutoka sekta mbalimbali leo wamekutana jijini Dar es Salaam ili kujadili namna ya kumlinda mlaji kutokana na matumizi ya akilia bandi (mnemba) ikiwemo ufanyaji biashara kwa njia ya mtandao.
Akizungumza katika kongamano la matumizi ya akili mnemba yanayozingatia haki na uwajibikaji kwa mlaji, Mkurugenzi wa Tume ya Ushindani(FCC) William Erio amesema sasa kila kitu inafanywa kwa njia ya mifumo ya kimtandao kwahiyo huduma nyingi zinatolewa na akili mnemba.
“Kwasababu hatuwezi kuepuka matumizi ya akili mnemba tulizani ni vyema kuwa na kongamano hili ambapo wataalamu wa mifumo kutoka sekta mbalimbali wataeleza ufahamu wao wa akili mnemba na namna inavyotumika.
Amesema wadau hao watawaambia ni kwa jinsi gani FCC inaweza kumlinda mlaji ikiwemo uwepo wa kanuni na sheria ambazo zinazingatia kumlinda mlaji wakati wa matumizi ya akili mnemba .
“Tunaangalia hii akili mnemba katika upangaji bei inaangalia haki kwa mlaji hayo tutazingatia mfano unapokata tiketi ya ndege bei unayopata ni sahihi na huduma ziko,”amesisitiza.
Ameongeza “Kama kuna kikwazo cha kisheria hatua stahiki tutachukua kupitia taratibu za serikali kuhakikisha matumizi ya akili mnemba yanatambulika kisheria na walaji wanalindwa.
Erio amebainisha kuwa wameendelea kutoa elimu kwa walaji kuhusu huduma zinazotolewa na akili bandi.
Mgeni rasmi katika kongamano hilo ambaye ni Mwenyekiti wa FCC, Dk Aggrey Mlimuka amesema
kongamano hilo linajumuisha wadau kutoka maeneno mbalimbali ikiwa ni pamoja na TEHEMA,Vyuo Vikuu,Taasisi za utafiti ,afya ,sera na sheria pamoja na wafanyabiashara kutoka sekta mbalimbali.
Amesema watajadili dhana ya akili mnemba na kwa jinsi gani mlaji anapaswa kulindwa dhidi ya changamoto mbalimbali zinazoweza kusababishwa na teknolojia hiyo.
“Matumizi ya akili mnemba katika utoaji huduma yanaweza kuathiri kwa kiasi kikubwa mfumo wa maisha ya walaji ambao pia ndio wananchi wa kawaida tunaowahudumia kama vyombo vya usimamizi wa uchumi wa soko.
Ametaja maeneno yanayotakiwa kupewa kipaumbe katika kulinda afya ya mlaji kuwa ni uundwaji wa mifumo huduma inayotumia akili mnemba,kubainisha athari na faida zake na uwajibikaji ambapo serikali kuweka utaratibu wa kiudhibiti wa watoa huduma na changamoto zinazoweza kujitokeza.
“Sote tunashauku ya kuboresha na kurahisisha utoaji wa huduma kwa ubora kwa walaji kwa kutumia teknolojia kama nyenzo muhimu kwa ustawi wa maslahi ya walaji na uchumi kwa ujumla .
Amesema azma hiyo itakuwa na maana pale mifumo hiyo ya kiteknolojia itazingatia uwajibikaji ,tija ,haki na usawa kwa kuwekewa mifumo thabiti ya usimamizi na udhibiti.
Naye Mwenyekiti wa baraza la ushindani, Jaji Salma Maghimbi amasema lazima wawe sehemu mu.himu kwa kuangalia teknolojia ili kumlinda mlaji kwani mambo mengo yanafanywa kupitia teknolojia hiyo
“Ninachowasihi dunia inakwenda mbele lazima tujue haki zetu kama walaji kuna watu wanapata vitu ambavyo hawakuagiza na wapo watu wanatapeliwa kufanya vitu mitandaoni,”amesisitiza.