Fedha za kijiji ‘zapotea’ Ofisi ya Maliasili Wilaya

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara,  Abdulrahman Kinana ametoa wiki moja kwa ofisi ya Maliasili Wilaya ya Itilima, kurejesha fedha Sh  milioni 11 za maendeleo ya Kijiji cha Mbogo.

Kinana pia amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Dk Yahaya Nawanda na Mkuu wa Wilaya ya Itilima Faiza Salum kuhakikisha fedha hizo zinarejeshwa haraka na kupewa ripoti.

Agizo hilo la Kinana limekuja baada ya Mwenyekiti wa Kijiji cha Mbogo, Ntimba Mahangila kudai kuwa maofisa maliasili walimpelekea fomu na kumtaka asaini kukiri kuwa kapokea pesa za maendeleo ya Kijiji Sh milioni 16 wakati fedha hizo hazijaingizwa kwenye akaunti ya kijiji.

“Mheshimiwa Mwenyekiti leo hii ungekuta nimefungwa  iwapo ningekubali kusaini, lakini niligoma nikasema mpaka nikahakikishe benki kweli fedha zimeingizwa, kufika benki kiasi nilichokikuta ni Sh 16,000 tu.

” Fedha hizo Sh milioni 11 zilipaswa kuingizwa kwenye akaunti tangu mwezi wa nne, lakini mpaka sasa hakuna hela yoyote na nimefuatilia mara kadhaa ni chenga chenga, sasa Mheshimiwa Mwenyekiti hizo hela tutazipata lini? ” Amehoji.

Akizungumzia hilo Kinana alimbana ofisa maliasili, ambaye alikiri kuwepo kwa suala hilo na kwamba watalishughulikia.

Kufuatia hali hiyo, Kinana akaagiza zirudishwe upesi ndani ya wiki moja na waliohusika wachukuliwe hatua. 

“Ofisa Maliasili Wilaya anasema badala ya hela kuingia akaunti ya Kijiji zikaingia akaunti nyingine, kuna jambo, msingesema zingeishia mifukoni mwa watu,” amesema Kinana.

Naye Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), Richard Kasesera amewataka watu waliopata mamlaka kuacha kulaghai, kunyanyasa na kuonea wananchi..

“Rais wetu mama Samia Suluhu Hassan anafanya kazi kubwa ikiwemo kujenga miundombinu ya shule, barabara  na hospitali, vyote hivi vitakua havina maana kama mnaonea wananchi, mnanyanyasa wananchi , mnawatolea lugha chafu wananchi.

” Hatutaki kuja hapa kusaka kura tusikie kero kama tunazozisikia, tusikie mnawatolea watu lugha chafu za maudhi, hatutavumilia tena, tutawashughulikia,” amesema.

Habari Zifananazo

5 Comments
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button