MBEYA: KIUNGO wa Azam fc Feisal Salum ‘Feitoto’ amefunga bao moja kwenye ushindi wa timu yake wa mabao 3-1 dhidi ya Ihefu Fc na kuwahakikishia waajiri wake alama tatu muhimu za ligi kuu Tanzania bara.
Msimu uliopita Feisal akiwa na kikosi cha Yanga alipitia maumivu ya Ihefu kwa kuwahariabia rekodi yao ya kutopoteza katika michezo 49, licha ya kwamba nyota huyo hakuwa sehemu ya kikosi kilichoivaa Ihefu katika mchezo huo uliopigwa Novemba 29, 2022.
Kiungo huyo anaesifika kwa uwezo wake wa kupiga mashuti ya mbali ana historia nzuri na Ihefu kwani alipokutana na timu hiyo Julai 15, 2021 akiwa na Yanga alifunga mabao mawili katika ushindi wa mabao 2-0 mchezo uliopigwa Uwanja wa Benjamini Mkapa, hivyo ni kama mchezaji huyo ameendelea pale alipoishia dhidi ya Ihefu.
Mabao mengine ya Azam fc katika mchezo huo wa leo yamefungwa na Sospter Bajana aliyefunga mabao mawili.
Matokeo hayo wamewapeleka matajiri hao wa kusini mwa Dar es Salaam hadi nafasi ya kwanza kwenye msimamo baada ya kushuka dimbani mara tisa wakiwa na alama 19.