Fidia hutolewa watumishi magonjwa ya milipuko

DODOMA; SERIKALI imesema huwa inatoa fidia kwa watumishi wa afya waliofariki kwa sababu za kuwahudumia wagonjwa wa milipuko na magonjwa mengine hatarishi.

Pia imesema hakuna mtumishi wa afya aliyekimbia kwa ajili ya kuogopa kuhudumia mtu mwenye magonjwa hatarishi au ya milipuko.

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu na Naibu wake, Dk Godwin Mollel wametoa kauli hiyo kwa nyakati tofauti bungeni mjini Dodoma kutokana na maswali ya Mbunge wa Viti Maalum, Jacquiline Msongozi.

Advertisement

Katika swali la msingi mbunge huyo alitaka kujua lini serikali itatoa fidia kwa madaktari na Manesi wanaopoteza maisha wakihudumia wagonjwa wa magonjwa ya mlipuko, ambapo katika majibu yake Naibu Waziri Mollel amesema serikali inatambua na kujali mchango mkubwa wa watumishi wanaohudumia wagonjwa wa milipuko wakiwemo madaktari na wauguzi.

“Napenda kulifahamisha Bunge lako tukufu kwamba serikali hutoa fidia kwa watumishi waliofariki kwa sababu za kuwahudumia wagonjwa wa magonjwa ya milipuko kwa Sheria ya Fidia kwa wafanyakazi Sura ya 263 marejeo ya Mwaka 2015 kupitia Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi Tanzania. Fidia zinazotolewa ni pamoja na gharama za mazishi na pensheni kwa wategemezi,” amesema Naibu Waziri.

Katika swali la nyongeza Mbunge huyo alihoji kwa nini serikali isiongeze motisha kwa watumishi wanaohudumia magonjwa hatarishi na ya milipuko, ambapo Naibu Waziri amesema hilo limekuwa likifanyika na kutolea mfano kwa daktari aliyepata changamoto ya afya wakati akimuhudumia mgonjwa wa Marburg mkoani Kagera, ambaye alipatiwa pole ya Sh milioni 10.

Waziri Ummy naye akasimama kutoa ufafanuzi kuhusu daktari huyo wa Kagera, kisha kusisitiza kuwa watumishi wa afya nchini wamekuwa mstari wa mbele kusaidia wagonjwa bila woga yanapotokea magonjwa ya mlipuko na hakuna ambaye amekimbia.

Amesema kipaumbele cha serikali ni kuwalinda watumishi wa afya katika masuala ya magonjwa hatarishi na ya mlipuko, ambapo miongoni mwa mambo hayo ni kuwapa mafunzo ya kuwahudumia wagonjwa na kuwapa vifaa kinga kwa ajili ya kuhudumia wagonjwa.

7 comments

Comments are closed.

/* */