Fifa yaifungulia pingu Yanga

DAR ES SALAAM: SHIRIKISHO la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) na Shirikisho la Mpira wa miguu Tanzania (TFF) wameiondololea klabu ya Yanga kizuizi cha uhamisho wa wachezaji.
Kupitia taarifa yake kwa umma, Ofisa Habari wa TFF, Cliford Ndimbo leo amesema uamuzi huo umefikiwa baada ya Yanga kukamilisha malipo ya aliyekuwa mchezaji wake Gael Bigirimana raia wa Burundi.
Awali mchezaji huyo alifungua kesi FIFA dhidi ya klabu hiyo ya Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kushindwa kumlipa baada ya kumvunjia mkataba.
Bigirimana alishinda kesi hiyo, na Yanga ilitakiwa kumlipa ndani ya siku 45 tangu uamuzi huo wa FIFA ulipotolewa, lakini haikutekeleza na kusababisha ifungiwe kusajili.
Yanga ilitangaza kumsajili Bigirimana katika dirisha la usajili la Julai 2022 na kuachana kwa mizengwe. Mchezaji huyo amewahi kuhudumu katika vilabu kadhaa vya Ulaya ikiwemo Newcastle United ya Uingereza na Rangers ya Scotland.

Habari Zifananazo

Back to top button