MWANASIASA chipukizi wa upinzani ambaye pia ni msanii wa muziki wa rege, Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine anatarajia kuzindua filamu yake katika Mji wa Venice nchini Italia, filamu hiyo inaeleza maisha yake ndani ya siasa za Uganda.
Filamu hiyo inayoitwa ‘Rais wa Getto’ inaonyesha kipindi cha mpito cha Bobi Wine kutoka kuwa mwanamuziki maarufu wa mitindo ya rege hadi kuwa mgombea maarufu wa urais nchini Uganda anayempa changamoto Rais Yoweri Museveni.
Mwanasiasa huyo amekuwa mpinzani mkubwa wa Rais Museveni hususani katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2021 ambapo Rais Museveni alishinda kwa asilimia 58 ya kura zote zilizopigwa katika uchaguzi huo.
“Siku zote nimekuwa nikitaka mambo yabadilike. Na hata katika muziki wangu wote nilikuwa nikiimba kuhusu mabadiliko chanya, mabadiliko ya tabia, Fikra za VVU na Ukimwi, usafi wa mazingira na haya yote yalitibuliwa miaka 15 iliyopita nilipovamiwa na maafisa wa usalama na kupigwa kwa sababu tu nilikuwa na gari zuri na kupendwa na wasichana,” alisema Bobi Wine.
Katika filamu hiyo, Bobi Wine anasema baada ya kupigwa makofi na watu wa usalama aliulizwa kuwa kwanini anajionyesha kama vile hajui kuwa nchi ina wamiliki wake hali ambayo anasema itakuwa ngumu kumtoka kichwani mwake.