Filamu ya Samia, Dk Mwinyi kuzinduliwa China

DAR ES SALAAM; FILAMU mpya ya kuitangaza Tanzania iitwayo ‘Amazing Tanzania’ inatarajiwa kuzinduliwa rasmi mwezi huu jijini Beijing, China ikiwashirikisha marais Samia Suluhu Hassan na Dk Hussein Mwinyi wa Zanzibar.

Katibu Mkuu,Wizara ya Maliasili na Utalii ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Rais ya Kutangaza Tanzania, Dk Hassan Abbasi alisema hayo katika kipindi maalumu na Wasafi FM mbashara kutokea Hifadhi ya Taifa ya Arusha kilichofanyika juzi usiku katika moja ya maeneo iliporekodiwa filamu hiyo.

Alisema Rais Samia mara ya mwisho wakati wa uzinduzi wa Filamu ya Tanzania: The Royal Tour, Dar es Salaam, alisema kazi hiyo itaendele. Alisema wengi walidhani kuwa itakuja The Royal Tour sehemu ya pili au hadi ya tatu.

“Lakini maana yake ilikuwa kazi ya kuitangaza Tanzania kwa ukubwa ule itaendelea,” alisema. “Leo (juzi) tuko hapa Hifadhi ya Taifa Arusha, eneo muhimu ambalo Rais Samia amefanya filamu nyingine
kubwa itakayoitangaza Tanzania duniani…,” alisema.

Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi

Alisema filamu hiyo, imefanyika katika hifadhi ya Arusha ambako kuna maeneo yamefanywa na Rais Samia na mengine Dk Mwinyi. Alisema filamu itagusa maeneo mengine ya dunia kwa kuzingatia mkakati uliopo.

“Kwanza filamu hii ina utofauti kidogo na Royal Tour pamoja na Rais Samia kuwa mhusika pia ameshiriki msanii maarufu wa China Jin Dong pamoja na Dk Mwinyi,” alisema.

Alisema itakuwa na maudhui mapya badala ya kuwa na mtangazaji kama ilivyokuwa Royal Tour itakuwa na msanii Jin Dong ambaye atapitishwa na Rais Samia katika maeneo mbalimbali ya utalii nchini.

Kuhusu sababu za uzinduzi kufanyika China, alisema ni taifa lenye idadi kubwa ya watu duniani wanaofikia bilioni 1.5, lakini pia wachina zaidi ya milioni 200 kwa mwaka hutoka kwenda sehemu mbalimbali duniani.

“Hii ni filamu ya kimkakati kwa ukubwa wa soko la China lakini pia nchi hii kwenye teknolojia ni kubwa Mashariki ya Kati,” alisema.

Alisema filamu hiyo inaanzia Zanzibar ambako Dk Mwinyi ameshiriki kisha Rais Samia amerekodi akiwa hifadhi ya Arusha. Itaonesha eneo la madini ya tanzanite na maeneo mengine ya ndani na lugha zilizotumika ni Kiswahili, Kiingereza na Kichina.

Alisema baada ya uzinduzi wa filamu hiyo Beijing, itaoneshwa katika miji ya Shanghai na Guangzhou na baadaye maeneo mengine yatatangazwa. Filamu hiyo ya kuitangaza Tanzania ni ya pili ikitanguliwa na Tanzania: The
Royal Tour ambayo mhusika wake mkuu ni Rais Samia aliyeeizindua jijini New York, Marekani.

Baada ya uzinduzi huo, hapa nchini ilizinduliwa Arusha Aprili 28 ikifuatia Zanzibar Mei 7 na kuhitimishwa kitaifa Dar es Salaam, Mei 8, 2022 Rais Samia alianza kurekodi filamu hiyo Agosti 29, 2021 kwa lengo la kuitangaza Tanzania kimataifa kupitia vivutio vya utalii. Kuzinduliwa kwa filamu hiyo kunatajwa kuchangia ongezeko la wawekezaji na watalii nchini.

Habari Zifananazo

Back to top button