Filamu yachangia ajira 30,000 kwa mwaka

Filamu yachangia ajira 30,000 kwa mwaka

SEKTA ya filamu imeweza kuchangia ajira takribani 30,000 ndani ya mwaka mmoja wa 2021, huku uwekezaji katika sekta hiyo ukizidi kuongezeka.

Haya yameelezwa leo jijini hapa na Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania, Dk Kiagho Kilonzo, alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu majukumu ya bodi hiyo.

Amesema kwa kipindi cha Januari hadi Desemba, 2021 pekee,  sekta hiyo inakadiriwa kuchangia takriban ajira 30,000 zilizotokana na filamu, ikijumuisha waigizaji, waandaaji na watoa huduma.

Advertisement

Amesema kiasi hicho ni ongezeko la nafasi 5,000 kutoka 25,000 kiasi kinachokadiriwa kuzalishwa mwaka 2020.

“Kwa mazingira ya Kitanzania, filamu moja ina wastani wa watu 20, tamthilia moja ina wastani wa watu 100,” amesema.

Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu nchini, Dk kiagho Kikonzo akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dodoma. (Picha na Iddy Mwema).

Akizungumzai mitaji na uwezeshaji kwenye sekta ya filamu, Dk Kilonzo amesema kumekuwepo na ongezeko kubwa la uwekezaji kutoka sekta binafsi.

Akitoa mfano anasema kwa mwaka 2021,Kampuni ya Azam Media iliwekeza takriban Sh bilioni 4 kwenye eneo la filamu pekee, ikiwa ni ongezeko la Sh bilioni 1 kutoka mwaka 2020, ambapo iliwekeza takriban Sh bilioni 3, ambazo ni katika ununuzi wa filamu, udhamini kwenye uandaaji wa filamu.

Alisema kwa mwaka 2020, Multichoice Tanzania iliwekeza takriban dola za Marekani milioni 3 katika kudhamini uandaaji na ununuzi wa filamu za kitanzania.

Kuhusu msoko na usambazaji wa filamu, Dk Kilonzo amesema, serikali imeendelea kuwawekea mazingira wezeshi kwa wadau wa filamu kujiajiri, hivyo kuongeza na kukuza pato la Taifa, kupunguza umaskini na kuchochea maendeleo ya sekta nyingine mtambuka kama vile utalii.

/* */