‘Flyover’ yanukia makutano Mwenge, Morocco

DODOMA; SERIKALI inaendelea na mazungumzo na Shirika la Maendeleo la Japan (JICA) kwa ajili ya ujenzi wa barabara za juu katika makutano ya Mwenge na Morocco jijini Dar es Salaam.

Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi kwa wizara yake kwa mwaka wa fedha 2024/25 bungeni mjini Dodoma leo, amesema miradi mbalimbali imefanyika nchini ili kukabiliana na msongamano wa magari barabarani.

“Katika kukabiliana na changamoto ya msongamano wa magari katika Jiji la Dar es Salaam, Serikali inatekeleza miradi ya ujenzi wa barabara za juu (Flyovers), ambapo ujenzi katika makutano ya TAZARA, Ubungo, Uhasibu na Chang’ombe umekamilika.

Advertisement

“Mazungumzo na Serikali ya Japan kupitia Shirika lake la Maendeleo la JICA yanaendelea kwa ajili ya ujenzi wa barabara za juu katika makutano ya Mwenge na Moroco.

“Vilevile, ujenzi wa miundombinu ya mabasi yaendayo haraka Awamu ya I kutoka Ubungo hadi Kivukoni umekamilika na awamu ya pili kutoka City Center – Mbagala unaendelea na umefikia Asilimia 99.

“Awamu ya tatu kutoka City Center – Gongo la Mboto umefikia Asilimia 26.55, awamu ya nne kutoka City Center – Tegeta kazi zimeanza na awamu ya tano kutoka Ubungo – Bandarini na Segerea – Tabata – Kigogo, zipo hatua za mwisho za manunuzi.

“Aidha, katika mwaka wa fedha 2024/25 Serikali itaanza upanuzi wa barabara ya Mwai Kibaki na Mbagala – Vikindu,” amesema Waziri Bashungwa.