Fountain Gate waipa 5 Tamisemi ujio Tahasusi mpya

MWANZA; MKURUGENZI Mtendaji wa Taasisi ya Fountain Gate Academy, Japhet Makau amemwandikia barua ya pongezi Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Mohammed Mchengerwa kwa uamuzi wa kuongeza Tahasusi (Combination) mpya 49, kutoka 16 zilizokuwepo awali hadi kufikia Tahasusi 65.

Tahasusi hizo mpya zitakazoanza kutekelezwa Julai, 2024 zipo katika makundi saba (7) ambayo ni Tahasusi za Sayansi ya Jamii, Tahasusi za Lugha, Tahasusi za Masomo ya Biashara, Tahasusi za Sayansi, Tahasusi za Michezo, Tahasusi za Sanaa, na Tahasusi za Elimu ya Dini.

Makau kwenye barua yake ameonesha wazi kufurahishwa na maamuzi hayo ya serikali na wizara kwa ujumla na kuongeza kuwa amekua mdau mkubwa hapa nchini kwa huduma ya elimu, michezo na sanaa kwenye Taasisi za Shule kwa miaka 17 .

Advertisement

Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dodoma katika mkutano ulioongozwa na Mkuu wa Shule za Fountain Gate Academy Joseph Msafiri, Mkurugenzi huyo amesema kuwa Fountain Gate Academy Mwanza  itakuwa shule ya kwanza kutelekeza maagizo hayo.

Meneja wa Mahusiano ya Kimataifa wa kituo hicho, Denis Joel na mratibu wa Fountain Gate Princess Issa Liponda (Issa Mbuzi), walithibitisha dhamira ya Makau ya kuunga mkono juhudi za serikali na kwanini aliamua kuandika barua hiyo kwa Waziri Mchengerwa.