Fursa bwerere soko la Ulaya, Watanzania waambiwa

Balozi wa Tanzania Ubelgiji, Luxembourg na Umoja wa Ulaya (EU), Jestas Nyamanga

BALOZI wa Tanzania Ubelgiji, Luxembourg na Umoja wa Ulaya (EU), Jestas Nyamanga ametaja fursa katika kilimo, biashara, utalii, uvuvi na uwekezaji zinazopatikana katika nchi hizo na kuwataka Watanzania kuzichangamkia.

Balozi Nyamanga alisema Tanzania inauza zaidi katika nchi hizo za Ulaya hususani Ubelgiji minofu ya samaki, dagaa, mazao ya parachichi, kakao, mbogamboga, pilipili, mchele kutoka Mbeya na biashara ya utalii.

Aliyasema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari kwa njia ya mtandao wa Zoom iliyoratibiwa na Taasisi ya Watch Tanzania.

Advertisement

“Ubelgiji ni nchi chache za Ulaya ambazo Tanzania tunauza zaidi kuliko tunavyonunua kwa takribani miaka minne mfululizo sasa. Tumekuwa tukiuza Januari hadi Mei, mwaka huu kiasi cha Euro milioni 81.6 ni zaidi ya wao ambao waliuza Euro milioni 75.2 kwetu,” alisema Balozi Nyamanga.

Alitaja bidhaa ambazo zina soko kubwa nchini humo kuwa ni minofu ya samaki aina ya sangara kutoka Mwanza ambayo jumla ya tani 50 mpaka 60 zinaingizwa nchini humo kutoka Tanzania kila wiki.

“Na endapo tutajipanga vizuri kiuzalishaji na ubora, kuna uwezekano wa kuingiza hadi tani 200 za minofu ya kila wiki kwa sababu demand (uhitaji) ni kubwa sana,” alisema Balozi Nyamanga.

Pia alisema soko la dagaa limefunguliwa hasa wa Kigoma na mahitaji yake ni makubwa, kiasi ubalozi umekuwa ukihamasisha pia na dagaa wa maeneo mengine wakiwamo wanaovuliwa katika maji moto na Zanzibar baada ya kubaini uwepo wa mahitaji makubwa.

“Tunauza pia mchele wa Mbeya ambao ni soko jipya, kuna mahitaji ya tani 300 kila mwaka ya mchele wa Mbeya, tunafanya uhamasishaji wa michele mingine ili nayo iingie katika soko,” alisema.

Kuhusu zao la kakao, alisema pia wameanza kuliuza katika soko la Ulaya likitokea maeneo ya Kyela, Mbeya na Morogoro na jitihada ni kuongeza uzalishaji ili Ulaya iwe soko kubwa la Tanzania.

Alisema katika soko la Ulaya, nchi inayoongoza kununua kakao ni Ubelgiji. “Tumepata kampuni moja iko tayari kununua tani za kakao 5,000, tunasihi sana Watanzania wanaoweza kuzalisha kakao isiyotumia kemikali wazalishe kwa wingi soko lipo,” alieleza.

Pia, aliwaelekeza Watanzania wanaotaka kuuza zao hilo Ulaya kuwasiliana na Taasisi inayojishughulisha na mbogamboga na matunda (Taha) yenye makao makuu Arusha ili kupata maelekezo ya kulifikia soko hilo.

Kuhusu zao la parachichi ambalo Tanzania ni ya tatu kuuza Ulaya zao hilo, ikitanguliwa na Afrika Kusini na Kenya, alisema nalo lina soko kubwa Ulaya ambako parachichi moja linauzwa Euro nne (zaidi ya Sh 10,000).

Pamoja na hayo, alizungumzia fursa ya kuuza Ulaya mazao ya pilipili na samaki aina ya migebuka.

Hata hivyo, alisema pamoja na uwepo wa fursa hizo kuna changamoto katika bandari za Tanzania baada ya wadau kubainisha kuwa bidhaa zinachelewa sana na zile zinazoharibika zinafika zikiwa zimeharibika.

Alisema eneo la utalii lina fursa nyingi kwa kuwa raia wa Ubelgiji kupendelea kutembelea Tanzania hasa Zanzibar.

Akizungumzia uwekezaji wa Ubelgiji nchini, alisema nchi hiyo ni miongoni mwa nchi 10 zilizowekeza zaidi Tanzania na ina miradi 45 yenye thamani ya Euro milioni 78 inayotekelezwa nchini katika maeneo mbalimbali ikiwamo katika Kampuni ya Bia Tanzania (TBL).

“Na katika kuendelea kuwekeza, tumezungumza na kampuni ya TBL ili kuanzisha kiwanda cha kimea kitakachogharimu kiasi cha Dola za Marekani milioni 50 na kitajengwa Dodoma,” alieleza.

Aidha, alisema pamoja na ushirikiano wa kirafiki na kiuwekezaji, mpaka sasa Ubelgiji ina ushirikiano wa ubia na nchi 14 tu duniani katika maendeleo ikiwamo Tanzania.

“Katika ubia huo, Ubelgiji imekuwa ikisaidiana na Tanzania katika miradi mbalimbali na wamekuwa wakitoa karibu Euro milioni 11 kila mwaka kupitia serikali na Asasi zisizo za Kiserikali (NGOs) zao,” alifafanua Balozi Kamanga.

Akizungumzia Luxembourg, alisema Watanzania wanaweza kunufaika na fursa ya mikopo ya bei nafuu kwani inaongoza katika masuala ya fedha Ulaya.

“Tunasihi kampuni na mashirika yanayotaka mikopo wawasiliane na benki kubwa waunganishe na benki za Luxembourg. Pia nchi hii pamoja na kuwa na miradi tisa yenye thamani ya Euro milioni 160 nchini ikiwemo kampuni ya Tigo, pia inatoa fursa ya elimu,” alisema.