Fursa za Bomba la Mafuta EAC zinasubiri Watanzania

HIVI karibuni Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padri Charles Kitima, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Jude Thaddaeus Ruwa’ichi na Askofu wa Jimbo Katoliki la Geita, Flavian Kassala, walizungumza na waandishi wa habari kuhusu Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP).

Walikuwa nje ya mkutano baina ya TEC na wataalamu wa EACOP kufafanua utekelezaji wa mradi kwa kuzingatia utunzaji wa mazingira, haki za binadamu na manufaa kwa taifa walipoungana na wadau wengine kuzitazama fursa lukuki zinazowasubiri Watanzania kupitia EACOP.

Mradi huu kutoka Uganda hadi Tanga, una urefu wa kilomita 1,443 kati ya hizo, kilomita 296 zipo Uganda huku kilomita 1,147 zikiwa Tanzania katika mikoa ya Kagera, Geita, Shinyanga, Tabora, Singida, Dodoma, Manyara na Tanga.

Walisema baada ya ufuatiliaji na ufafanuzi, wamebaini na kuridhika kuwa, mradi una manufaa kwa Watanzania na taifa kwa ujumla.

Wakataka Watanzania wauunge mkono na kuchangamkia fursa zilizo katika mradi huo wakisisitiza kuwa, Kanisa limeridhishwa na mchakato, tahadhari na kuzingatiwa kwa haki za binadamu na uhifadhi wa mazingira katika utekelezaji.

Ndio maana ninasema, wakati Watanzania wakipaswa kupuuza watu, taasisi au nchi zinazopinga mradi huo kwa sababu malengo na maslahi binafsi tofauti na ukweli na hali halisi, watambue kuwa EACOP kuna fursa lukuki zinazowasubiri Watanzania.

Wapuuze watu wanaopinga EACOP bila sababu za msingi na zenye ushahidi wa kisayansi, badala yake wachangamkie fursa kadiri zinavyojitokeza.

Binafsi, nawapongeza viongozi hao wa dini na wadau wengine kwa kuchunguza na kusema ukweli hadharani mintarafu faida za EACOP na namna mradi huo unavyozingatia haki za binadamu na kuchukua tahadhari kubwa dhidi ya uharibifu wa mazingira.

Nijuacho mimi, licha ya kuzingatia tafiti za kisayansi, mradi huu unatoa fursa mbalimbali za kiuchumi na kibiashara katika hatua za awali za mradi, wakati wa ujenzi na wakati wa uendeshaji ambazo watu wa mataifa mengine wasingependa Watanzania wazipate baada ya wao kukosa mradi huo.

Kwangu mimi, faida hizo ni pamoja na kufanya marekebisho ya mazingira pale ambapo Watanzania tuliyaharibu kwa shughuli zetu zikiwamo za uchimbaji madini pamoja na kuuza bidhaa na huduma mbalimbali zikiwamo za chakula kwa wafanyakazi na bidhaa zitakazohitajika wakati wa utekelezaji zikiwamo za ujenzi.

Fursa nyingine ni ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja.

Ndio maana ninasema, EACOP ni mradi wenye fursa zinazowasubiri Watanzania. Wajiunge na kufanya ‘umoja’ wenye nguvu za kibiashara ili wanufaike zaidi.

1 Comment
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button