Gabo Zigamba azindua Tamthilia ya “Baraluko”

MSANII nguli wa filamu nchini Tanzania, Salim Ahmed maarufu kama ‘Gabo Zigamba’, amezindua rasmi tamthilia yake mpya iitwayo “Baraluko”, akieleza kuwa ni kazi ya kipekee itakayobadilisha mwelekeo wa tasnia ya filamu nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Gabo amesema tamthilia hiyo inalenga kuonyesha maisha halisi ya Mtanzania na kuhamasisha ufuatiliaji wa kazi za ndani miongoni mwa watazamaji wa Kitanzania.

“Katika tamthilia hiyo nimeshirikisha wacheza mpira wa miguu ambao wanafanya vizuri zaidi kwa sasa.”

“Jambo lolote ukiweka kwa uangalifu linaweza kuwa zuri. ‘Baraluko’ imeandaliwa kwa ubora wa hali ya juu na naamini itabadilisha mtazamo wa watu kuhusu tamthilia zetu,” amesema Gabo.

“Tunalenga kuwafikia mashabiki wetu wote, kuwaburudisha na kuwaelimisha kwa kutumia maisha ya kila siku ya Mtanzania kama msingi wa simulizi.”

Gabo alieleza kuwa tamthilia hiyo inashirikisha wasanii waandamizi pamoja na chipukizi, ikiwa ni jitihada za kukuza vipaji vipya sambamba na kuendeleza wakongwe katika tasnia hiyo.

“Baraluko” itaanza kurushwa rasmi kupitia YouTube channel ya Gabo Zigamba kuanzia Jumatano, ikiwa ni njia ya kufikia watazamaji wengi zaidi kwa urahisi.

Kwa upande wake, Mary Mtemi, ambaye amecheza kama Veronika ndani ya tamthilia hiyo, amesema kuwa kazi hiyo imetengenezwa kwa viwango vya juu na itatosheleza kiu ya watanzania kwa burudani halisi.

“Kupitia ‘Baraluko’ tumeweza kushibisha ile njaa ya watanzania ya kuona tamthilia zenye maudhui halisi. Tumejivunia kuonyesha uzuri wa nchi yetu kwa kurekodi katika mikoa mbalimbali ya Tanzania,” amesema Mary.

Ameongeza kuwa tamthilia hiyo inaangazia zaidi masuala ya mapenzi, na itakuwa ikirushwa kila baada ya siku tano. Vilevile, timu ya watayarishaji imepanga kufanya ziara katika vyuo vya sanaa ili kuwahamasisha vijana na kushiriki uzoefu wa utendaji wa kazi kwa vitendo.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button