SERIKALI ya kijeshi nchini Gabon imetangaza uchaguzi wa rais na wabunge utafanyika mwezi Agosti 2025, kulingana na ratiba itakayoidhinishwa na mkutano wa kitaifa mwezi Aprili 2024.
“Agosti 2025: uchaguzi na mwisho wa kipindi cha mpito”, alitangaza msemaji wa nguvu za kijeshi moja kwa moja kwenye televisheni ya serikali Gabon Première, akiorodhesha ratiba rasmi ya mpito iliyopitishwa na Mkutano wa Baraza la Mawaziri.
“Ratiba lazima iwasilishwe kwa kongamano la kitaifa ikiwa ni pamoja na wahusika muhimu wa taifa lote lililopangwa kufanyika Aprili 2024.” Aliongeza.
Ali Bongo, 64, ambaye alitawala nchi hiyo tangu 2009, alipinduliwa na viongozi wa kijeshi mnamo Agosti 30, muda mfupi baada ya kutangazwa mshindi katika uchaguzi wa rais, ambao jeshi na upinzani walitangaza kuwa ni udanganyifu.
Waziri mkuu mpya wa Gabon, Raymond Ndong Sima amesema kuwa kipindi cha mpito cha miaka miwili kabla ya uchaguzi huru kilichoahidiwa na watawala wapya wa kijeshi nchini humo kilikuwa na malengo thabiti.