Gachagua: Serikali itaboresha mitaala

NAIBU Rais Rigathi Gachagua amesema serikali mpya haitafutilia Mtaala wa Umahiri (CBC), bali itaupitia ili kuuboresha.

Akizungumza katika Tamasha la Kitaifa la Muziki lililofanyika katika Shule ya Upili ya Wasichana ya Kisumu, Naibu Rais Gachagua alisema serikali itaunda kikosikazi kuchunguza matatizo na dosari zilizopo katika mtaala uliopo na kuyashughulikia. Kikosi kazi kitashauriana na wadau husika katika sekta ya elimu wakiwemo wazazi.

“Hivi karibuni serikali itazindua kikosikazi cha kuangalia mageuzi ya kielimu ikiwa ni pamoja na mitaala ya umahiri, si kwa nia ya kuifuta, bali kuipitia upya ili kuhifadhi mazuri yaliyomo na kuboresha mambo yenye dosari,” alisema Gachagua.

Naibu rais alisema pia kuwa, utawala wa Kenya Kwanza utajihusisha na uchumi wa ubunifu ili kuhakikisha unabuni nafasi za kazi na mapato kwa vijana wenye vipaji.

“Serikali ina sera na programu za kutafsiri vipaji vya vijana wetu kuwa mapato,” alisema.

Gachagua aliwaambia Wakenya kuwa, utawala wa Rais William Ruto utawatumikia Wakenya wote kwa usawa na bila kujali tofauti za kisiasa.

“Tunataka kuwathibitishia watu wa Nyanza kwamba, utawala wa Ruto utahudumia Wakenya wote kwa usawa, wale waliotuchagua na wale ambao hawakutuchagua,” alisema.

“Sehemu zote za Kenya zitapata maendeleo kwa usawa kwa sababu sisi ni viongozi wa nchi nzima,” aliongeza.

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button