Gambo asifu usaidizi wa nabii kwa jamii
MBUNGE wa Jimbo la Arusha Mjini, Mrisho Gambo amesema utajiri wa Nabii Mchungaji Geor Davie unasaidia Jamii wakiwemo Vijana, Wanawake na Walemavu na kuwataka Matajiri wengine kuiga mfano wa nabii huyo katika kusaidia Jamii.
Gambo alisema hayo nyumbani kwake jana wilayani Arumeru mkoani Arumeru wakati akisherehekea siku yake ya kuzaliwa iliyohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa dini na serikali.
Alisema wafanyabiashara wa soko la Samunge lililopo katikati ya Jiji la Arusha vijana na wanawake walipewa zaidi ya shilingi Millioni 100 na Nabii Davie na pia alitoa zaidi ya shilingi milioni 20 kwa ajili ya ujenzi wa uzio wa soko hilo na kuweka mageti ya kuingilia sokoni hapo.
Mbunge huyo alisema kuwa hizo ni jitihada chache zinazoonekana kwa jamii lakini bado amekuwa akifanya hivyo kwa mtu mmoja mmoja bila kujali dini wala kabila hivyo aliwaasa wafanyabiashara wengine Jijini Arusha na Mkoa kuinga mfano wa Nabii huyo.
Naye mke wa Geor Davie, mchungaji Anna Davie amemuomba Gambo kutatua changamoto ya barabara ya Likamba iliyopo kata ya Kisongo Arumeru yenye umbali wa zaidi ya km 5 inayopitwa na wakazi zaidi ya 5000 kwani barabara hiyo imekuwa mbovu kupitika hususani kipindi hiki cha masika.
Alisema njia hiyo hupitwa na wakazi zaidi ya 5000 wa eneo la Kisongo kwa nyakati zote lakini kwa sasa kipindi cha mvua hali ni mbaya na wakazi wa eneo hilo wanapata taabu sana katika muda huu wa mvua kubwa.
“Naomba sana Mh mbunge tusaidie juu ya ukarabati wa barabara hiyo ikiwezekana pia fikisha maombi yangu kwa Mh Rais Mama yetu Samia Suluhu Hassan juu ya hii changamoto ya barabara kwani wakazi wa Kisongo ambaoi ni wakulima na wafugaji na wanategemea barabara hii kusafirisha mifugo yao kupeleka mnadani pamoja na kusafirisha mazao yao” Alisema Mchungaji Anna Davie .
Mara baada Maombi hayo Mbunge Gambo alisema amepokea maombi hayo na kuahidi kuyafanyia kazi ikiwa ni pamoja na kuwafikishia wataalamu wa idara ya Barabaara Vijijini TARURA.
Nabii Davie aliwashukuru wageni wote waliofika katika sherehe hiyo maalumu ya siku yake ya kuzaliwa na kusema kuwa kufika kwao kumemfariji na kuonyesha kuwa wanaupendo kwake.
Alisema yeye kama Mtumishi wa Mungu yuko kwa ajili ya kusaidia jamii yote iwe usiku au mchana na ataendelea kufanya hivyo kwa muda wote bila ya kusukumwa na mtu yoyote kwani uamuzi huo unasukumwa na Mwenyezi Mungu na mtu au watu.