Geita Gold haitanii usajili mpya

MKURUGENZI wa Halmashauri ya Mji wa Geita, Zahara Michuzi amesema wamejipanga kufanya usajili bora wa wachezaji na benchi la ufundi na kuboresha maslahi ili timu ya Geita Gold irejee kwenye ubora.

Michuzi amesema hayo katika mahojiano maalum na HabariLeo na kueleza wanatambua mchango wa wachezaji na benchi la ufundi la Geita Gold kwa msimu uliopita lakini wamejipanga kujiimarisha zaidi.

Amesema maboresho ya kikosi cha Geita Gold FC yanaenda sambamba na uharakishaji mradi wa ujenzi wa mpira wa Magogo ili kutoa nafasi kwa mashabiki kushuhudia mechi zote za Geita Gold uwanjani hapo.

“Tunalichukua kwa umuhimu wake na kwa uzito wake, kuhakikisha tunaenda kusajili benchi zima la ufundi zuri, benchi ambalo tunaliwekea malengo.

“Malengo ambayo yanatakiwa yafikiwe ndani ya miezi sita, na kama hayajafikiwa tutatimuana, iwe asubuhi, iwe jioni, moto ni uleule.” Amesema na kuongeza;

“Lakini pia tunaboresha pia maslahi, kwa maana ya maslahi ya benchi la ufundi, maslahi ya walimu wote, mwalimu mkuu na wasaidizi wake, maslahi pia ya wachezaji pamoja na watumishi wote ndani ya timu.

“Huko kote tunaenda kuboresha kuhakikisha timu hii inaleta tija na kufikia adhima ya serikali ya kuwapatia wananchi ajira ambayo itakuwa inawahakikishia mshahara kila mwezi.”

Ameeleza, pia wamejipanga kuzalisha jezi bora na za kutosha tofauti na msimu uliopita ambapo kampuni waliyoingia nayo ubia na imewahakikishia jezi hizo zitawasili mapema mwezi Agosti mwaka huu.

“Mpaka sasa mkandarasi anakamilisha ‘kit’ ya tatu, ‘kit’ ya kwanza na ya pili zipo kwenye uchapishaji, zikikamilika zitaanza kuja na meli na ‘kit’ ya tatu itafuata, tukikamilisha zote zitakuwa sokoni.

“Kilichotufanya msimu ulipita tukakosa jezi rasmi ya kuchezea, ni misukosuko wanaotuzalishia jezi kuchelewesha jezi kufika hapa nchini, kwa hiyo suala hili tumelichukua kwa tahdhari kubwa.”

Habari Zifananazo

Back to top button