TIMU ya Geita Gold FF inayomilikiwa na halmashauri ya mji wa Geita imezindua mpango wa kusajili wanachama wa klabu, lengo likiwa ni kuwafanya wanachama kuwa sehemu ya umiliki wa klabu.
Ofisa Mtendaji wa klabu, Simon Shija amesema hayo leo Februari 21, 2023 kwa waandishi wa habari na kueleza hatua hiyo itasaidia kuongeza mapato ya klabu kwa kila mwanachama kulipia kadi kwa kila mwezi.
Amesema mpango huo unatekelezwa kwa mujibu wa katiba ya klabu na utatoa fursa kwa Watanzania wenye mapenzi na timu ya Geita Gold ndani na nje ya mkoa wa Geita kupata kadi za uanachama.
“Kwa mjibu wa katiba ya Geita Gold ibara ya tano, inazungumuzia wanachama, kwa hiyo tunawapa nafasi pana sasa kuanza kuiendesha klabu yao na kuweza kuichangia.
“Tunakwenda kuzindua kadi za uanachama, tunakwenda kuzindua matawi sehemu mbalimbali, matawi hayo yataweza kuchangisha michango mbalimbali kwa ajili ya klabu,” amesema na kuongeza;
“Kwa mujibu wa katiba ya Geita Gold ibara ya 10, inazungumuzia ada za wanachama, ambapo kwa mwezi kila mwanachama ataichangia kadi 3,000.”
Ameeleza, matarajio ya awali ni kusajili wanachama 2,000 ndani ya mkoa wa Geita na kupata angalau sh milioni 72 kwa mwaka itakayoongeza mapato ya klabu ambayo ni wastani wa Sh bilioni 1.6.
Shija ameweka wazi mpango huo utarasimisha wanachama kumiliki asilimia 49 ya hisa za klabu huku halmashauri ikisalia na asilimia 51 za umiliki wa hisa za klabu ya Geita Gold.
Aliongeza, ili kufikia malengo klabu imeingia mkataba na kampuni ya N-Card kwa ajili ya kutengeneza kadi za wanachama na timu inatarajiwa kucheza michezo ya kirafiki vijijini kuhamasisha wananchi.