‘Geita ipangwe kisasa’

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Abdulrahman Kinana amezitaka Halmashauri ya Mji wa Geita na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita kusimamia ujenzi unaoendelea mjini Geita ufanyike kwa mipango na tija.

Kinana alitoa maelekezo hayo alipotembelea baadhi ya miradi ya kimkakati ndani ya Halmashauri ya mji wa Geita.

“Pangeni mji, wekeni maeneo yenu vizuri, hata ikiwezekana wekeni fedha kwenye kupanga mji kwanza, kitu gani kikae wapi, ukiona jengo la bluu pale unajua ni la Ofisi ya Uhamiaji, ofisi zote za serikali zikae maeneo ambayo ni karibu karibu,” alisema na kuongeza:

Advertisement

“Kuna kitu kinaitwa ‘huduma senta’ yaani ukitoka kwa Mkuu wa Mkoa unaenda kwa Mkuu wa Uhamiaji, kwa TRA (Mamlaka ya Mapato Nchini), sasa pangeni huu mji vizuri, ukae vizuri kabisa watu waanze kusema ukitaka kuona mji mzuri nenda Geita.”

Kinana alieleza kutofurahishwa na hali ya mwonekano na utimamu wa taa za barabarani mjini Geita ambazo nyingi zimeonekana kutotoa mwanga kutokana na ubovu na kuagiza hatua za haraka zichukuliwe kumaliza kero hiyo.

“Huwa napenda kutoa mfano wa Rwanda, kwa waliowahi kufika Rwanda, hakuna taa ambayo haiwaki, hakuna balbu ambayo imezimika, mpaka vijijini wameweka taa zao lakini zinawaka sasa unajiuliza nani huyo anayesimamia mpaka taa zote zikawaka,” alisema na kuongeza:

“Lakini sisi mambo yetu kuna uswahili ndani, ukiuliza utaambiwa tupo kwenye mchakato, ukiuliza utaambiwa tuko mbioni, ukiuliza zaidi utaambiwa fedha hazijaja, ukiuliza zaidi utaambiwa tutalifanyia kazi, basi majibu rahisi kwa mambo magumu.”

Ofisa Mpango Mji wa Halmashauri ya Mji wa Geita, Barbara Mustafa alisema tayari wameweka mwongozo kuhakikisha ujenzi unaofanyika unazingatia taratibu na ramani ya mji wa Geita.