TIMU za Bunda Queens, Geita Gold Queens, Mwanza Queens na JMK Park zimetinga nusu fainali ya mashindano ya ligi ya mabingwa ya mkoa kwa ligi ya wanawake inayoendelea mjini hapa.
Michezo yote minne ya robo fainali ilichezwa jana kuanzia asubuhi.
Bunda ilifikia hatua hiyo kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Singida Warriors. Bao pekee la mchezo huo lilifungwa na Jamila Celestine katika dakika ya 19.
Geita ilifika hatua hiyo kwa kuifunga Ruangwa Queens mabao 3-0. Na JMK Park iliingia nusu fainali baada ya kushinda kwa mabao 2-0 dhidi ya Masala Princess na Mwanza Queens ikiifunga Mount Hanang mabao 2-1. Hiyo yote ilichezwa jana katika viwanja vya shule ya Alliance.
Kwa matokeo hayo Geita itacheza nusu fainali dhidi ya Bunda huku Mwanza ikicheza na JMK Park.
Mechi za nusu fainali zinatarajiwa kuchezwa leo asubuhi.
Kocha mkuu wa Geita, Joseph Charles alipongeza wachezaji wake kwa kushinda mchezo wao wa robo fainali dhidi ya Ruangwa queens.
Alisema mchezo haukuwa mwepesi bali wachezaji wake walipambana kwa kufuata maelekezo muda wote.
Alisema wamejipanga vyema kushinda mchezo wao wa nusu fainali dhidi ya Bunda.
Amewaomba wapenzi wa soka mkoani Geita waendelee kuiunga mkono timu yao ifike fainali na kutwaa ubingwa.