TIMU ya soka ya Geita Gold, imeondoka jana kueleka Sudan kwa ajili ya mchezo wake wa raundi ya kwanza ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Hilal Alsahil FC unaotarajiwa kuchezwa kesho.
Katika kikosi cha wachezaji 25 kilichosafiri, mshambuliaji wao tegemeo George Mpole atakosekana kwenye mchezo huo unaotarajiwa kuchezwa mji wa Khartoum. Kwa mujibu wa Ofisa Habari wa Geita, Hemed Kivuyo Mpole alisema hajisikii vizuri wakiwa kwenye maandalizi ya safari hiyo juzi usiku.
“Mpole amebaki kwasababu timu ikiwa kwenye maandalizi ya safari alisema hajisikii vizuri kwa hiyo hakusafiri,”alisema Kivuyo.
Kikosi kilichosafiri kinaongozwa na benchi la Ufundi Kocha Mkuu Fred Minziro na Msaidizi wake Wandiba Mathias, Mkurugenzi wa Ufundi Lucas Mlingwa, Meneja Msabaha Salehe na Waziri Mahadhi, daktari Edger Rison na Kocha wa magolikipa Malindi Augustino.
Wachezaji ni Kelvin Yondani, Omary Ibrahimu, Bakari Hussein, Adeyum Salehe, Mbegu Yahya, Kidikilo Chars, Jonathan Mwaibindi, Sebusebu Samsoni, Mac Arakaza, Danny Lyanga, Raymond Masota, George Wawa, Okoyo Cosmas, Offen Chikola, Chombo Ridondo, Kelvin Nashon na Eric Yema.
Geita baada ya kucheza mchezo huo wa kwanza inatarajia kurudi nyumbani kujiandaa na mchezo wa marudiano utakaochezwa Septemba 17, mwaka huu.