WABUNIFU wa mitindo na mavazi mjini Geita wameanzisha tamasha la maonesho ya sanaa na mavazi, ‘Golden Fashion Festival’, ili kuunga mkono juhudi za kuvutia watalii zilizoanzishwa na Rais Samia Suluhu Hassan katika filamu ya Royal Tour.
Mratibu wa tamasha hilo, Mkurugenzi wa Kampuni ya Mitindo ya Kasikana Collection, Bertha Komba amesema uzinduzi rasmi utafanyika Machi 3, 2023.
Amesema tamasha hilo litatumika kama jukwaa la kuibua vipaji vya wabunifu wapya wa mitindo kutangaza kazi za wabunifu wabobezi kutoka mikoa ya kanda ya ziwa, ili kupanua uwigo wa fursa sekta ya sanaa.
Amesema tamasha litasaidia kuhimiza jamii kuipa thamani biashara ya ubunifu na kuondoa dhana potofu iliyojengeka ndani ya jamii kuamini kwamba kazi ya mitindo na ushonaji siyo rasmi kwa vijana.
“Mbali na kazi ya sanaa ya ubunifu na mitindo, jukwaa hili linatoa fursa ya kuwatangaza wajasiriamali wote wa bidhaa zinazohusiana na mitindo ikiwemo nguo, viatu, shanga, vito vya madini.
“Niwafahamishe, jukwaa hili la Golden Fashion Festival tutalitumia kutafuta wabunifu wa mavazi na mitindo, ili kazi hizi za ubunifu ziende kutumika pia kuvutia watalii kama ilivyo kwa Royal Tour,” amesema.
Amesema malengo ya awali ni kupata wana mitindo takribani 30 mkoani Geita, ambao wataenda kuuwakilisha mkoa kwenye tamasha kubwa la maonesho ya mitindo litakalofanyika Desemba 2023.
Mbunifu chipukizi, Rose Titto amekiri kupitia tamasha hilo watapata nafasi ya kujitangaza na kuonesha uwezo wao katika sekta ya sanaa na kupanua uwigo wa kuendelea kuaminika wanapojiajiri.
Mwanamitindo chipukizi, Hans Brown ameiomba jamii kuachana na dhana potofu juu ya sekta ya mitondo, badala yake waendelee kuwaunga mkono wanamitindo kwani ni sehemu ya ajira.