Geita wavutiwa bima ya afya kwa wote

Geita wavutiwa bima ya afya kwa wote

MENEJA wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), mkoani Geita, Elias Odhiambo, amesema wananchi wengi wanaotembelea maonesho ya tano ya teknolojia ya madini mjini Geita wameonesha nia ya kupata uelewa juu ya mpango wa bima ya afya kwa wote.

Odhiambo amesema hayo, wakati akizungumza na waandishi wa habari katika banda la NHIF, viwanja vya Bombambili mjini Geita na kueleza wanaendelea kutoa elimu juu ya mpango huo, ili kila Mtanzania apate uelewa.

“Watu wamefika kwa ajili ya kupata elimu ya bima na wengine wanaenda kukamilisha taratibu za kujiunga, lakini wengi wamekuwa na shauku kubwa kujua ule mpango ambao serikali inaenda kuanzisha, mpango wa bima ya afya kwa wote.

Advertisement

“Kwa hiyo wamefika hapa wakataka kuuliza, tumewapa taarifa chache ambazo tunazo, kama mnavyofahamu ni kwamba utaratibu mzima bado upo bungeni kwa ajili ya kukamilisha taratibu za kisheria.

“Lakini tahimini ambayo nimeiona mwitikio na shauku ya wananchi kutaka kujua mpango wa bima ya afya kwa wote utaanza lini, ni mkubwa sana hasa kwa jinsi ambavyo watu wanafika kwenye banda letu kuuliza,” amesema Odhiambo.

Daktari wa kitengo cha magonjwa ya nje bima kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Geita, Dk Groly Temba, aliwashauri Watanzania kuitikia mpango wa bima ya afya kwa wote kutokana na changamoto kubwa ya magonjwa yasiyoambukizwa.

Amesema zaidi ya asilimia 80 ya Watanzania, waliotembelea banda la NHIF na kupima afya zao, wamebainika kuwa na magonjwa yasiyoambukizwa yaliyochagizwa na uzito uliopitiliza kutokana na mfumo wa maisha.