Geita yavunja rekodi ulipaji kodi

Wapania makubwa zaidi mwakani

GEITA: MAMLAKA ya Mapato Nchini (TRA) mkoani Geita imefanikiwa kukusanya kiasi cha Sh bilioni 55.07 kwa mwaka wa fedha 2022/23 sawa na ufanisi wa asilimia 142.7 ya lengo la makusanyo ya Sh bilioni 38.59.

Makusanyo hayo ni ongezeko la Sh bilioni 20.68 ukilinganisha na makusanyo ya Sh bilioni 34.39 zilizokusanywa mwaka 2021/22 na kufanya ukuaji wa makusanyo kwa mwaka kufikia asilimia 60.

Kamishina wa Kodi za Ndani TRA, Alfred Mregi amebainisha hayo wakati akizungumza katika hafla ya kuhitimisha wiki ya mlipa kodi mkoani Geita iliyoambatana na utoaji tuzo kwa walipakodi.

Amesema kupanda kwa kiwango cha makusanyo ya kodi ni matokeo ya kuwa na jamii ya walipakodi wazalendo wanaohamasika na wanaojitoa kwa dhatii na kwa vitendo.

“Tunaposherehekea mafanikio tuliyoyapata katika mwaka wa fedha wa 2022/23 tunakumbushwa pia umuhimu wa kujenga misingi imara zaidi ya utendaji katika mwaka wa fedha ujao.

“Kwa mwaka huu wa fedha 2023/24 kwa mkoa wa Geita tunalo lengo la kukusanya Shi bilioni 44.18, ni matarajio yetu kwamba tutafanya jambo kubwa zaidi pengine kuliko la mwaka jana.”

Mkuu wa mkoa wa Geita, Martin Shigela alielekeza makundi yote matatu kuanzia mlipaji, mkusanyaji na mtumiaji wa kodi kufanya kazi kwa pamoja ili kupanua uwigo wa ukusanyaji wa kodi.

Ameelekeza wasimamizi wa mapato ya serikali kuhakikisha fedha zinaenda sehemu stahiki na zinatumika kwa ufasaha ili walipa kodi waone matunda ya kodi zao na kuongeza hamasa ya uwajibikaji.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chemba ya Wafanyabiashara Nchini (TCCIA) mkoa wa Geita, Mhandisi Robert Gabriel amewaomba wafanyabiashara kuunga mkono juhudi za serikali kwa kutunza kumbukumbu zao za biashara.

 

Habari Zifananazo

Back to top button