Geita yavutia wawekezaji kutoka Dubai

KAMPUNI ya Isra Gold Tanzania inayomilikiwa na wawekezaji kutoka Dubai, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) imefungua kituo cha kusafisha dhahabu mkoani Geita chenye thamani ya Sh bilioni 4.2.

Uwekezaji huo ni matunda ya ziara ya Rais wa Tanzania, Dk Samia Suluhu Hassan nchini UAE Februari 2022 ambapo alipata fursa ya kutembelea na kuinadi Tanzania kwenye maonesho ya Dubai Expo 2022.

Akizungumza mwishoni mwa wiki katika uzinduzi wa kituo hicho kilichopo kata ya Lwamugasa wilayani Geita, Mkurugenzi wa  Isra Gold Tanzania, Mostaq Ahmed amesema wamevutiwa na sera rafiki ya uwekezaji nchini Tanzania.

Amesema kituo (kiwanda) hicho kitafanya kazi ya kusindika udongo wenye madini ya dhahabu na kitakuwa na uwezo wa kusafisha tani 15 za dhadhabu kwa saa, ambapo kitafanya kazi kwa muda wa saa 24.

Amebainisha uwekezaji huo ni mwanzo, na malengo ni kujenga vituo vingine vitano kabla ya mwaka huu kuisha na pia kuongeza vituo vingine 10 ndani ya mwaka 2024 ili kufikia jumla ya vituo 16.

Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martin Shigella (katikati) akishuhudia makabidhiano ya cheti cha uwekezaji kati ya Mkurugunzi Mtendaji Kituo cha Uwekezaji Nchini (TIC), Gilead Teri na viongozi wa Kampuni ya Isra Gold Tanzania.

Mkurugenzi Mtendaji wa Isra Gold Tanzania, Ismael Van Der Schya amewahakikishia wakazi wa Geita kupata kipaumbele cha ajira na kwa kuanzia watatoa ajira 46 za mkataba na kuchangia miradi mbalimbali.

Mkurugunzi Mtendaji Kituo cha Uwekezaji Nchini (TIC), Gilead Teri ameeleza, wawekezaji hao wamefuata na kuzingatia kanuni na taratibu zote za kuwekeza nchini na kupatiwa cheti cha uwekezaji kutoka TIC.

“Wajibu wangu na watumishi wenzangu tutawezesha kupanua uwigo wa mradi huu, na kufanikisha mpango kazi wa uwekezaji ndani ya nchi yetu ili jamii  ya Geita na Tanzania nzima iweze kunufaika,” amesema.

Mkuu wa Wilaya ya Geita, Colnery Magembe amesema kwa kuwa uwekezaji huo utaenda kuongeza mapato ya halmashauri wilayani humo, atahakikisha wawekezaji wanalindwa na kupewa ushirikiano stahiki.

Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martin Shigella amekiri ziara ya Rais Samia kwenda Dubai Expo 2022 imefungua milango kwa wawekezaji sekta ya madini na mkoa umeweka mazingira rafiki kupokea wawekezaji kwenye sekta tofauti.

Habari Zifananazo

Back to top button