Gharama usafishaji figo kuwa Sh 90,000

SERIKALI ina mpango wa kupunguza gharama za usafisahi figo kutoka kiasi cha Sh 350,000 hadi Sh90,000.

Hayo yamesemwa bungeni Dodoma leo Jumatatu na Naibu Waziri wa Afya, Dk Godwin Mollel wakati akijibu swali la nyongeza kutoka kwa Mbunge Viti Maalum, Lucy Sabu aliyetaka kufahamu mpango wa Serikali wa kupunguza gharama za usafisaji figo [dialysis] ambazo zimekuwa kikwazo kwa watu wenye kipato kidogo.

“Hadi jana [Jumapili] kupitia bajeti hii tunayoiwasilisha sasa tulikuwa tunangalia mambo mawili. Waziri wetu [Ummy Mwalimu] alikuwa anaangalia eneo la mama na mtoto na eneo hili (dialysis).

“Tumebaini badala ya huduma hii kuwa Sh350,000 kuna uwezekano kabisa wa mtu kutibiwa kwa kati ya Sh 90,000 hadi Sh150,000 kwa hiyo tuna mpango wa kushusha gharama hizi,” Dk Mollel ameliambia Bunge.

Kuhusu msamaha wa matibabu hayo, amesema ikiwa mhitaji ana barua kutoka kwa mtendaji wako wa kata basi anaweza kupata msamaha wa gharama za usafishaji wa figo.

Kabla ya kauli hiyo ya Serikali, Mbunge wa Viti Maalum, Lucy Sabu alihoji maswali ya nyongeza akitaka kujua mambo ya kuzingatia ili mtu wa kipato cha chini aweze kupata msamaha wa matibabu hayo.

Akizungumzia juu ya utaratibu, Dk Mollel amesema endapo mtu akiwa na waraka huo kutoka ngazi ya kata, basi utaratibu wa msamaha unafanyika.

Awali, Naibu Waziri aliwaeleza wabunge kuwa kwa sasa huduma hiyo inapatikana katika hospitali mbalimbali hapa nchini ikiwemo Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Hospitali za rufaa za kanda na mikoa pamoja na ile ya Chuo Kikuu cha Dodoma.

Habari Zifananazo

Back to top button