GISELA KIMARIO : Kamanda Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori

GISELA Kimario
  • Anayeonesha njia katika ulimwengu unaomilikiwa na wanaume

GISELA Kimario ni miongoni mwa makamishna wasaidizi waandamizi watano pamoja na makamishna wasaidizi 12 waliotunukiwa vyeo na Amiri Jeshi Mkuu Rais Samia Suluhu Hassan Aprili 9, mwaka huu.

Alikuwa miongoni mwa waliopata maarifa ya kitaalamu na mafunzo maalumu na kisha kuvalishwa vyeo hivyo na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania, Meja Jenerali mstaafu, Hamisi Semfuko kwa niaba ya Amiri Jeshi Mkuu, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Gisela ambaye ni Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) baada ya kutunukiwa cheo hicho  aliteuliwa kuwa Kamanda wa Uhifadhi wa Kanda ya Ziwa.

Advertisement

Nafasi hiyo inamfanya Gisela kuwa mwanamke wa kwanza na pekee katika nafasi ya Makamanda wa Kanda kwa upande wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania.

Anasema utumishi wake ulianza miongo kadhaa katika Idara ya Wanyamapori, idara ambayo ilianzishwa kipindi cha ukoloni.

GISELA akipongezwa

Miaka minne baada ya kuajiriwa na aliteuliwa kuwa Meneja wa yaliyokuwa Mapori ya Akiba Burigi, Biharamulo na Kimisi yaliyopo mkoani Kagera.

Anasema uteuzi huo ulimfanya pia kuwa mwanamke wa kwanza na pekee kutumikia nafasi ya meneja wa mapori tangu kuanzishwa kwa Idara ya Wanyamapori na baadaye kuanzishwa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania.

Gisela alianza kuajiriwa kwenye sekta ya uhifadhi akiwa Ofisa wanyamapori daraja la pili mwaka 2005 na kupangiwa kufanya kazi dawati la utalii katika mapori ya akiba ya Burigi, Biharamulo na Kimisi.

Kwa mujibu wa Gisela wakati anaanza kazi alikuwa mwanamke pekee kati ya watumishi zaidi ya 30 waliokuwa wakifanya kazi kwenye mapori hayo.

“Hii inaonesha kuwa bado katika kipindi hicho wanawake walikuwa wachache katika sekta ya uhifadhi… ni kutokana na mazingira ya kazi kuwa porini na kuhusisha matumizi ya silaha za moto hivyo kufanya kazi hiyo kuonekana ni ya wanaume zaidi,” anasema Gisela.

Lakini katika mazingira hayo, anasema alimudu kufanya kazi na hata walipoajiriwa wanawake wengine na kupangiwa katika kituo hicho walifanya kazi vizuri kwa kufuata nyayo zake.

Gisela anasema katika safari yake ya utumishi, mwaka 2011 alihamishiwa kwenda kwenye Mfuko wa Kuhifadhi Wanyamapori Tanzania na alifanya kazi kama Ofisa Miradi wa Mfuko huo.

“Nilikitumikia cheo hicho hadi nilipohamishiwa na kupelekwa kufanya kazi kwenye Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania mwaka 2019,” anasema Gisela.

Anasema hii ni baada ya serikali kufanya mabadiliko katika Idara ya wanyamapori iliyoanzishwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania.

Mamlaka hii ilianzishwa kwa ajili ya kutekeleza majukumu ya ulinzi wa rasilimali za wanyamapori kwenye maeneo yote yaliyopo nje ya Hifadhi za Taifa na eneo la Hifadhi ya Ngorongoro.

Mwalimu Julius Nyerere katika moja ya hotuba yake ya mwaka 1961 aliwahi kunukuliwa katika nukuu hii maarufu ya Azimio la Arusha akisema, “uhai wa wanyamapori ni jambo linalotuhusu sote Afrika, viumbe hawa wa porini, wanapokuwa kwenye mapori wanamoishi sio tu kwa ajili ya kuajabiwa na kuvutia lakini pia ni sehemu ya maliasili yetu na pia ndivyo mustakabali wa maisha yetu ya baadaye. Kwa kukubali dhamana ya wanyamapori wetu tunataka kwa dhati kwamba tutafanya kila tuwezalo kuhakikisha kwamba wajukuu wa watoto wetu wataweza kufurahia urithi huu mkubwa na wa thamani na adimu.

“Mapori ya Akiba na maeneo yote yenye mapori huhitaji maarifa ya kitaalamu, wafanyakazi waliopata mafunzo maalumu na fedha. Hivyo tunaomba mataifa mengine yashirikiane nasi katika kazi hii muhimu, ambayo kufanikiwa au kutofanikiwa kwake hakuathiri tu Bara la Afrika bali ulimwengu mzima kwa ujumla.

Gisela anasema baada ya kuanzishwa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania, Idara ya Wanyamapori ilibakia na majukumu ya sera na urekebu.

Anasema baada ya kuhamishiwa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania alipewa kazi ya kuratibu uandaaji wa mipango ya usimamizi wa maeneo yanayosimamiwa na Mamlaka hiyo.

Gisela anasema kazi hiyo ameifanya kwa weledi na ufanisi mkubwa mpaka alipoteuliwa kuwa Kamishna Msaidizi Mwandamizi.

Anasema baada ya kutunukiwa cheo ameteuliwa kuwa Kamanda wa Uhifadhi wa Kanda ya Ziwa ambayo ni mojawapo ya Kanda sita zinazosimamiwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania.

“Ninamshukuru Mungu sana kwa cheo na nafasi ya uteuzi niliyopata kwani ni bahati ya kipekee,” anabainisha.

Kwa mujibu wa Gisela, miongoni mwa majukumu atakayokuwa nayo ni kuimarisha ulinzi wa rasilimali za wanyamapori, mahusiano na wananchi, wadau mbalimbali na ukusanyaji wa mapato kutokana na shughuli za matumizi ya wanyamapori katika kanda hiyo.

Gisela anamshukuru Rais Samia kwa jinsi anavyoendelea kuthamini mchango wa wanawake na anatoa wito kwa wanawake kwa kusema: “Kazi yoyote ukiidhamiria, ukaweka nia na ukimtumainia Mungu inawezekana bila kujali jinsia.”

Taaluma

Gisela ana Shahada ya Wanyamapori kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam pamoja na Shahada ya Uzamili ya Mipango na Usimamizi wa Miradi kutoka Chuo Kikuu cha Bradford nchini Uingereza.

Alipata elimu ya sekondari katika Shule ya Mkuu Sekondari iliyopo mkoani Kilimanjaro na Shule ya Wasichana wenye vipaji maalumu ya Msalato, mkoani Dodoma.

Gisela ni mke na mama wa watoto wawili ambaye anajitahidi kuhakikisha anatekeleza majukumu yake ya kifamilia na kazi bila mojawapo kuathiri jingine.

Katika maisha nje ya kazi anajishughulisha na ujasiriamali na pia kumtumikia Mungu kwenye Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG).

4 comments

Comments are closed.