Giza, uhalifu unavyozorotesha uchumi wa usiku Dar

MARIJAN Mohamed Natenga anatayarisha meza yake ya muda kabla ya siku ya biashara. Muuza viatu huyu wa zamani katika Soko la Kimataifa la Kariakoo sasa anakaanga pweza. Anataka pweza awe thabiti, mkavu kiasi na laini na ili kufanikisha hilo anahitaji zaidi ya sufuria na nyama ya pweza.

Anasema wateja wengi wanataka pweza aliyekaangwa na bado laini na ili awe hivyo, inamchukua takribani saa 1 dakika 30 kila siku kumtayarisha. Kwa miaka 10 sasa, pweza imekuwa moja ya vyakula vinavyopendwa na maarufu vikiuzwa karibu kila kona ya barabara katika jiji kuu la kibiashara la Dar es Salaam.

Kawaida, chakula hiki hufurika barabarani nyakati za jioni hadi usiku. Wanaume wametambuliwa kama watumiaji zaidi wa ladha hii ya kupendeza, ambapo pia wanathibitisha huongeza hamu ya mapenzi na nguvu za kiume.

Lengo la Natenga ni kuhakikisha wateja wake wanaotembelea meza yake katika Mtaa wa Kwa Azizi Ally katika Manispaa ya Temeke wanaridhika kila wakati.

Baadhi ya vijana wakitembea kwa uvivu walipita meza ya Bw Natenga huku akihangaika kumkata pweza vipande vipande, bila kusumbuliwa na kelele za daladala, madereva wa pikipiki, na wapita njia.

Mahali hapa ni hai leo, hakika kutakuwa na usiku mzuri wa biashara, anasema huku akitayarisha kwa haraka pweza aliyekatwakatwa na viungo mbalimbali kwenye bakuli. Kadiri pweza anavyozidi kuwa na ladha, ndivyo anavyozidi kuwa mtamu na ndivyo Natenga anavyopata wateja wengi zaidi.

Ni wazi kwamba Natentaga ameridhika na biashara yake mpya. Ikilinganishwa na biashara yake ya awali ya kuuza viatu ambapo hakuwa na uhakika wa kupata mteja. Biashara ya pweza bila shaka inampa matumaini kwa kuwa na zaidi ya wateja 20 waaminifu ambao hufuata na kujipatia supu ama kutafuna vipande vya pweza kila siku baada ya kazi.

Natenga anaunganisha balbu yake kutoka kwenye duka la karibu ili kumulika meza yake. Siku ambazo hakuna umeme, biashara bado huendelea kwa Natenga, kwani anategemea taa ya mafuta kuangaza meza yake kama wafanyabiashara wengine wadogo.

Ni dakika 15 kufika saa tatu usiku, kwa saa za Dar es Salaam. Kwa wakazi wengi ni wakati wa kuwa nyumbani. Lakini kwa Natenga na wafanyabiashara wengine, ni wakati wa biashara. Kama vile Natenga, mama mmoja mwenye umri wa miaka 34 na mfanyabiashara mdogo, Asha Yahaya anasema: “Wateja wetu huwa ni watembea kwa miguu.

Meza ya Marijan Mohamed Natenga

Hilo linahusisha wale wanaotoka au wako kazini na wale ambao wana muda kuwa nje kwa sababu tofauti, tunawahitaji… ni tumaini letu pekee la kustawi katika biashara zetu za usiku.”

Asha anategemea kupika na kuuza chakula mtaani ili kugharamia mahitaji yake na ya watoto wake watatu ambao kwa sasa wako shuleni. Wakati wa mchana biashara yake inakabiliwa na vikwazo vingi kutoka kwa askari wa manispaa.

“Hali ni tofauti kwa jioni na haswa usiku. Ninaweza kuuza chakula changu kwa raha zaidi,” anasema, akiangazia kwamba yeye hufanya mauzo mengi kati ya saa tatu na saa saba usiku.

Kando ya mapambano kama hayo na mamlaka, biashara ya Asha kama biashara nyingine nyingi za usiku inapambana na imani kwamba huchangia uchafuzi wa mazingira na kusababisha kelele. Maeneo mengine ni kwamba biashara za usiku zinashindwa kukuwa kutoka na shughuli za kihalifu kama vile biashara haramu, unyanyasaji wa kijinsia na wizi.

Dk. Egidius Kamanyi wa Idara ya Sosholojia na Anthropolojia katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) hakubali kabisa dhana hii iliyotolewa na Asha.

Anaeleza: “Kuna baadhi ya watu wanaokwenda kazini kwa zamu lakini hakuna hata mmoja wao amewahi kuripoti kesi za wizi au unyanyasaji. Ndiyo watu wanahitaji kuwa na uhakika wa usalama wao lakini isiwe sababu pekee.”

“Uchumi wa usiku sio tu kuhusu dawa za kulevya, ukahaba, au vitendo vingine vya uhalifu,” alisema. “Uchumi wa usiku unakumbana na imani za utamaduni na miundombinu duni.” Kulingana na mtaalamu huyo, watu wengi huwa wanahusisha shughuli za usiku na uovu.

“Kwa mfano, ikiwa mwanamke anaenda au anatoka kazini nyakati za usiku, atahukumiwa kwa kuanza na familia yake, na mara nyingi kuitwa majina,” anasema. “Hii ni sawa na wanaume, lakini wanaume waliooa ndio waathirika zaidi.”

Mfamasia katika moja ya maduka ya matibabu, mita chache kutoka katika meza ya Asha, anaamini kuwa shughuli za kibiashara za usiku huongeza thamani zaidi kwa uchumi. “Tumeongeza muda wetu wa kufungua na tunafanya mauzo usiku na hivyo kulipa kodi zaidi,” alisema. Akisisitiza kuwa biashara nyingi zinategemeana. Alitoa mfano wa wauzaji wa chakula. Asha akiwa ni mmoja wa wanufaika wa uchumi wa usiku.

Mtaa wa Kwa Azizi Ally usiku saa 3:15

Salumu Bakari mwenye umri wa miaka thelathini na sita ni mchuuzi mwingine wa chakula katika eneo hilo. Kwa miaka minane amekuwa akikaanga Chips Kuku. Bakari anakiri, kumekuwa na mauzo zaidi baada ya kupanua biashara zake hadi saa za usiku. “Nilikuwa peke yangu lakini sasa nimeweza kuajiri wenzangu wanne kusaidia kuendesha biashara,” alisema.

Mteja ambaye alikataa kutajwa jina leke alisema yeye na mfanyakazi mwenzake hununua chakula kutoka mitaani karibu kila siku wanapotoka kazini. HabariLEO iliona baadhi ya watu ambao wanaweza kuwa wameoa hata hivyo wanapata supu kutoka kwa wachuuzi.

Bw Bakari, hata hivyo, ni mmoja kati ya maelfu ya wafanyabiashara wadogo wadogo wanaofanya maisha ya uchumi wa usiku Dar es Salaam. Meza yake ya muda ipo karibu na makutano ya barabara za Kilwa na Mbagala. Yeye na wafanyabiashara wengine huhudumia madereva, wasafiri na wapita njia.

“Chakula ndio kila kitu. Iwe usiku au mchana. Watu wanahitaji kula ili kufanya kazi ipasavyo na hilo ndilo ninalotoa,” alisema. “Nimeweza kujipatia Kipato cha kutosha kusaidia familia yangu na hata kufadhili elimu ya Chuo Kikuu ya dada yangu”.

Haikuwa rahisi kwa Bakari kukumbuka ni kiasi gani haswa hutengeneza nyakati za usiku. Lakini anasema kawaida ni zaidi ya kile anachotengeneza wakati wa mchana.

Ingawa wametawanyika, minyororo hii ya wafanyabiashara wadogo ina jukumu kubwa katika uchumi wa maisha ya usiku wa Dar es Salaam, kutoa bidhaa na huduma kwa wote licha ya changamoto nyingi zinazokabili biashara zao.

Kuhusu Uchumi wa Maisha ya Usiku

Huko Seattle, Marekani, uchumi wa usiku ulitengeneza asilimia 2.2 za ajira mwaka 2020 na kuwa sekta kubwa zaidi kutengeneza ajira. Katika mwaka huo huo huko New York, tasnia hiyo ilizalisha dola za Kimarekani bilioni 35.1 (karibu trilioni 81.85/- ) katika shughuli za kiuchumi, ikichangia zaidi karibu dola za Marekani milioni 700 (kama trilioni 1.6) katika mapato ya kodi ya ndani.

Uchumi wa maisha ya usiku ulichangia asilimia 8 ya jumla ya ajira, na kuifanya kuwa tasnia ya tano kwa ukubwa mnamo 2019 nchini Uingereza.

Mfanyabiashara mdogo Salum Bakari

Uchumi wa maisha ya usiku umekuwa muhimu sana katika nchi zilizoendelea. Huko Seattle kwa mfano, jiji liliteua meya wa usiku. Tangu 2016, mtetezi huyu wa maisha ya usiku alikuwa na jukumu la kusaidia kampuni kupata vibali na kuhakikisha hazikwamishwi kufanya biashara. 

Katika miaka ya hivi karibuni, miji mingi duniani kote imetambua kuwa uchumi wa wakati wa usiku unaochangamka una jukumu muhimu sio tu kusaidia ukuaji endelevu wa uchumi, lakini pia kwa kutoa mchango chanya kwa maisha na utamaduni wa watu.

Mchumi na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Zanzibar (ZU) Prof Haji Semboja ameiambia HabariLEO kwamba uchumi uliochangamka na  uliochanganyika wakati wa usiku unaweza kuhimiza utalii, kukuza uchumi wa ndani na kuchangia katika kujenga maeneo ambayo watu wanataka kuishi.

Anasema: “Shughuli hizi za usiku zinatawaliwa na mifumo ya kisheria na kitaasisi. Kadiri uchumi unavyoendelea ndivyo tofauti inavyopungua kati ya mchana na usiku.” Mfumo wa kitaasisi hapa unajumuisha mamlaka zilizopewa kazi ya kutoa leseni na kutoa vibali, operesheni za jeshi la polisi pamoja na mambo mengine.

“Changamoto katika nchi zinazoendelea kiuchumi kama Tanzania ni kwamba watu hawana taarifa za kutosha,” alibainisha. “Sio kuhusu wakati lakini aina ya biashara ambayo inakubaliwa kwa ujumla katika jamii.”

Takwimu zisizo rasmi zinaonesha kuwa asilimia 60 ya Pato la Taifa la Tanzania halijahesabiwa na kubaki kwenye sekta isiyo rasmi. Anitha James, mchambuzi wa sera jijini Dar es Salaam anakubaliana na Prof Semboja. Anasema Tanzania inahitaji mabadiliko ya kimfumo ili kusimamia wafanyabiashara wadogo hadi wakubwa.

“Wafanyabiashara wanapaswa kukubali kufuata sheria, wakati jamii pia ijifunze kuwakubali wafanyabiashara,” alisema akisisitiza. “Kitaifa, uchumi wa wakati wa usiku unatoa mchango mkubwa kwa uchumi na ajira.”

Shughuli katika Duka kubwa la Mlimani City zikiwa zimefungwa.

Ingawa hii inafaidi wazi, wataalam wanaonya kuwa uchumi wa usiku unaweza pia kuleta changamoto kwa jumuiya za mitaa. Dk. Kamanyi anaangazia kuwa uchumi wa usiku usiodhibitiwa vizuri unaweza kusababisha kuongezeka kwa uhalifu, tabia zisizo za kijamii, na matatizo mengine yanayoweza kuongeza shinikizo la ziada kwa polisi na huduma za dharura.

“Uchumi wa jioni unahitaji sera na miundo, sawa na uchumi wa mchana,” Bw Deo Shayo, Mchambuzi wa Biashara katika Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) alisema. Pia anakubali kwamba kuna haja ya kukuza uchumi wa wakati wa usiku ili kusaidia kuongeza ufanisi na tija.

Nchini Tanzania, kuenea kwa imani za kitamaduni, mgawanyiko wa kisheria, ukosefu wa usalama na miundombinu duni kumefanya miji kushindwa kuendesha uchumi wa usiku, na kusababisha hasara kubwa ya mapato ya serikali.

Miongoni mwa majiji matano nchini Tanzania, Dar es Salaam imekuwa ikifanya jitihada za kuendesha uchumi wa usiku.

SkyCity Mall ambapo duka kubwa la Jambo linafanyakazi karibu saa 24

Sasa kuna angalau Duka moja, Jumbo, ambalo linatoa huduma karibu saa 24. Uwanja wa Ndege, Hospitali na idadi ya wafanyabiashara na wafanyabiashara wadogo wanaweka uhai katika maisha ya usiku Dar es Salaam.

Maisha ya Usiku Dar es Salaam

Kwa zaidi ya miaka kumi sasa, Dar es Salaam imekuwa ikifanya jitihada kuwa mojawapo ya miji mikuu ya kisasa barani Afrika. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla, anaamini dhamira mpya ya serikali ya kurekebisha taa za barabarani na kamera za CCTV itasaidia kukuza mpango wa nchi kuendesha uchumi wa usiku.

Waangalizi, hata hivyo, wanasema mipango kama hiyo imekuwa kwenye karatasi tangu mwaka 1995. “Ninaamini tunasonga katika mwelekeo sahihi. Tuna majengo mirefu, miundo na barabara kadhaa zinazoangaza barabarani,” alisema Dk. Kamanyi. “Tatizo ni kwamba sheria ndogo za jiji zimekuwa sio za kudumu.”

Dk.Kamanyi alikuwa akizungumzia uamuzi ambao ulitolewa awali na mamlaka za mkoa ukioagiza baa zote zifungwe ifikapo saa 6:00 usiku. Uamuzi huo huo ulibadilishwa na haujafanana katika miji yote. Kwa upande mwingine jeshi la polisi linasisitiza biashara ya usiku kufungwa ifikapo saa 6:00 usiku.

Mtaa wa Samora jijini Dar es Salaam ukiwa gizani

Dar es Salaam ikiwa ni mojawapo ya miji inayokua kwa haraka, ina wakazi milioni 5.4, kulingana na matokeo ya sensa ya Agosti, idadi ya watu ikiwa imeongezeka kutoka milioni 4.4 mwaka 2012. Mwaka 2020, eneo hilo lilikuwa na Pato la Taifa la juu zaidi la takriban trilioni 25.3/- (dola za Marekani bilioni 10.9).

Takwimu hizo zinaweka Dar es Salaam kuwa jiji la pili kwa ukubwa kiuchumi Afrika Mashariki baada ya Nairobi.

Upangaji mbovu na uhaba wa miundombinu unaathiri kwa kiasi kikubwa ratiba ya Dar es Salaam kufurahia hali ya uchumi wa nyakati za jioni na usiku. Uchunguzi wa mdogo kwenye mitaa kadhaa inayoendesha biashara ya usiku unaonesha hakuna ufikiaji wa moja kwa moja wa umeme, bila kusahau vifaa vya kudumu.

Wakati maeneo mengi yanang’arisha meza zao kwa jenereta za gharama kubwa, wachuuzi wengi hutumia taa za mafuta ya taa na taa zinazoweza kuchajiwa tena.

Kuanzia utawala wa Rais John Magufuli hadi Rais Samia Suluhu Hassan, mamlaka zimekuwa zijidhatiti kuangaza jiji hilo. Takriban barabara zote za lami zinazojengwa sasa zinafungwa taa zinazotumia nishati ya jua. Mahojiano na wakaazi, hata hivyo, yalifichua kuwa bado kulikuwa na shida na taa, kwani kwa siku kadhaa taa huwa zimezimwa. Na hata zikiharibika inaweza kuchukua zaidi ya mwaka kurekebishwa. 

Mtaa wa Samora, kwa mfano, upo katikati ya jiji mita chache tu kutoka ilipo Ofisi ya Rais, Ikulu Magogoni. Kuna taa zimeharibika tangu uchaguzi mkuu 2020 hadi sasa miaka miwili baadaye hazijarekebishwa. Tarura, wasimamizi wa barabara ama jiji la Ilala hawana majibu.

“Tuna mradi ambao haujakamilika …ambao ni kuangaza mitaa yote ya Dar es Salaam na kurekebisha kamera za CCTV kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere hadi Kariakoo na Kati kati ya Jiji,” Mkuu wa Mkoa, Makalla alisema. Ili wafanyabiashara wafanye biashara 24/7, tumejenga masoko ya kisasa na tunakusudia kujenga zaidi ili wakazi waweze kupata masoko kwa saa nyingi zaidi.

Msemaji wa Polisi, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) David Misime anasema Jeshi la Polisi limeongeza doria katika jiji hilo ili kuhakikisha usalama wa watu na mali zao. “Pia tunashirikisha umma kwa ujumla kushiriki katika kuimarisha usalama … polisi hawawezi kuwa katika kila sehemu nchini kote,” alisema.

Natenga na Bakari, wafanyabiashara wawili wa usiku, wanasema ukosefu wa suluhu ya taa ya kudumu inaathiri sana biashara zao. Kwa mujibu wa Bakari, wafanyabiashara hao wadogo wamekuwa wakiunda vikundi vya kuchangia jenereta moja linalosaidia kumulika meza zao.

Asha Yahaya

“Mifumo ya kisheria na sera za kirafiki ni muhimu sana kwa uchumi wa usiku. Miundombinu, ikiwa ni pamoja na mwanga, inajenga mazingira ya usalama,” aliongeza Prof. Semboja wakati wa mahojiano na HabariLEO. Barabara nyingi bado ziko gizani.

Hivi karibuni Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson alikuwa na maoni kwamba ajali nyingi za barabarani zinaweza kusababishwa na ukosefu wa usafiri wa umma, hasa mabasi nyakati za usiku.

Kuikabili changamoto

Wafanyabiashara jijini Dar es Salaam wameiambia HabariLEO kuwa changamoto zilizopo hazijawazuia kuendesha uchumi wa usiku, kutengeneza ajira na kupanua uchumi.

“Umeme umekuwa tatizo hivi karibuni, lakini hatuwezi kukunja mikono. Tunasonga mbele na suluhu mbadala,” alisema Alex Massawe ambaye anaendesha klabu ya usiku mjini hapa. Waziri wa Nishati, January Makamba anakiri kuwa mabadiliko ya tabia nchi hivi karibuni yaliathiri mfumo wa umeme wa maji nchini.

Takwimu zilizochapishwa na Shirika la Umeme nchini (Tanesco) mwezi Novemba zilisema uwezo wa kuzalisha umeme umepungua kwa megawati 350 kutokana na kushuka kwa kiwango cha maji katika mabwawa ya kimkakati.

“Tunaamini tuna suluhu ya kudumu… Mradi wa Umeme wa Maji wa Julius Nyerere (JNHPP),” alisema Bw Makamba. Mradi huu wa megawati 2115 utaanza uzalishaji wa umeme mnamo 2025.

Salehe Ally, mhitimu wa chuo kikuu anayeendesha usafiri wa teksi Ubungo anasema umeme ndiyo kila kitu. “Kukiwa na umeme watu pia watakuwa nje ya kufanya kazi na tutakuwa tukipata biashara, zaidi ya hapo ni hali mbaya tu.”

Alisema baada ya kukosa kazi rasmi, udereva texi unamsaidia kujikimu kimaisha. Mjasiriamali mwingine, mwendesha bodaboda aliliambia habarileo kuwa usalama ni changamoto nyakati za usiku. “Inakuwa mbaya zaidi ikiwa taa imezimwa. Tunaogopa kuchukua watu lakini nao wanaogopa na kumekuwa na visa vya waendesha Bodaboda kuibiwa,” alisema. “Wateja pia huripoti matukio ya kushambuliwa.”

Bodaboda wengi walisimulia jinsi wenzao wamekuwa na matatizo wakati wa kazi zao nyingi usiku. Baadhi ya kesi pia zilithibitishwa na jeshi la polisi.

Msemaji wa jeshi la polisi SACP Misime amesema jeshi la polisi linashirikiana na jamii katika kusaidia kutokomeza vitendo vya uhalifu pamoja na unyanyasaji wa kijinsia katika jamii. “Tunaendesha mafunzo ya uhamasishaji wa umma kutoka shule za msingi hadi chuo kikuu kuhusu jinsi ya kugundua wahalifu,” alisema. Sasa, kuna madawati 420 ya jinsia kote nchini ambayo yanasaidia kushughulikia unyanyasaji wa kijinsia katika jamii.

Huku Dar es Salaam ikilenga kuwa uchumi wa maisha ya usiku ifikapo 2030, wataalam wanaitaka serikali kushughulikia masuala yanayokinzana ya sera ambayo yanaweza kuathiri kasi yake kuelekea uchumi wa juu wa maisha ya usiku wa kanda.

Kama huko Uingereza, Mchambuzi wa Sera Anita, anasema, kitaifa msimamo wa Serikali kuhusu burudani zinazohusiana na pombe umekuwa ukikinzana. “Wakati polisi wakitaka biashara ya burudani kufungwa ifikapo saa 6:00 usiku baadhi ya wakuu wa mikoa wanaona ni sawa kwa biashara kufanya 24/7. Hili ni tatizo,” alisema. Anapendekeza kwamba baraza la madiwani wa jiji lazima liunganishe sera zake na sera zingine za serikali.

Ulimwenguni kote, baa, vilabu vya usiku, wafanyabiashara wadogo ni ishara za maisha ya kijamii ya kila jiji. Dar Es Salaam, kama vile Miji mingine barani Afrika, inakua haraka kuwa sehemu kuu ya wazee na vijana, watalii na wasafiri wa biashara ambao wanataka kuungana na kuwa na wakati mzuri wa vinywaji, chakula na muziki. Kuwezesha taa na usalama kwa watoa huduma na watumiaji, bila shaka kutaimarisha tasnia ya uchumi wa maisha ya usiku.

Habari Zifananazo

Back to top button