Guinea Bissau, Morocco timu za kwanza kuwasili Ivory Coast

IVORY COAST: Timu za GUINEA Bissau na Morocco zimekua timu za kwanza kuwasili nchini Ivory Coast tayari kwa michuano ya Mataifa Afrika (AFCON) kwa mwaka 2023 zinazotarajiwa kuanza kutimua vumbi Januari 13, 2024.

Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) kupitia kurasa zake rasmi za mitandao ya kijamii ya X na Instagram  limetangaza taarifa hiyo ya kuwasili kwa timu hizo Januari 08, 2024.

Guinea Bissau itacheza mechi ya ufunguzi wa michuano ya AFCON 2023 dhidi ya mwenyeji Ivory Coast kabla ya kuvaana na Equatorial Guinea  na Nigeria katika mitanange ya kundi A.

Guinea Bissau imetoka kupoteza kwa  mabao 6-2 dhidi ya Mali kwenye mechi ya kirafiki iliyocheza Jumamosi mjini Bamako nchini Mali kabla ya kuanza safari ya kuelekea Ivory Coast.

Timu ya Taifa ya Morocco inatazamwa kama miongoni mwa timu zitakazofanya vizuri kwenye michuano hiyo ikiwa na historia nzuri ya kuishia hatua ya nusu fainali ya Michuano ya Kombe la Dunia, mwaka 2022 nchini Qatar.

Habari Zifananazo

Back to top button