Gwajima: Asilimia kubwa ukatili kwa watoto ni ndugu

WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dk Dorothy Gwajima amesema utafiti uliofanyika kuhusu ukatili dhidi ya watoto unafanywa na ndugu wa karibu.

Anasema utafiti unaonesha kwamba asilimia 60 ya ukatili kwa watoto hao unafanyika nyumbani ambapo ndugu na jamaa wa karibu wakihusika na asilimia 40 unafanyika nje ya familia ikiwamo shuleni.

Dk Gwajima alitoa takwimu hizo katika Kijiji cha Maya Maya wilayani Bahi mkoani hapa wakati wa maandalizi kuelekea maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Familia Duniani inayofanyika kila mwaka Mei 15.

Alisema changamoto kubwa dhidi ya ukatili wa watoto ni ukimya na kumalizana kimyakimya miongoni mwa wanafamilia na matokeo yake taarifa hazifikishwi kwenye vyombo vya sheria.

“Wazazi tumeacha njia ya malezi kwa watoto wetu ndio maana vitendo vingi vya ukatili dhidi ya watoto vinaripotiwa kutokea nyumbani, hii ni kwa sababu tumewaacha watoto wajilee wenyewe na hapo ndio wanashawishika na kuingizwa kwenye mitego ya kubakwa na kulawitiwa.”

“Mfano kwa mujibu wa taarifa ya polisi kuanzia Januari hadi Desemba mwaka 2022, matukio ya ukatili dhidi ya watoto yaliyoripotiwa ni 12,163 ambapo wasichana ni 9,962 na wavulana ni 2,201 ukilinganisha na matukio ya mwaka 2021 jumla yalikuwa 11,499 utagundua hapo kuna ongezeko la matukio 664 sawa na asilimia 5.8,” alisema.

Aidha, alibainisha kwamba matukio yaliyoongoza ni ya ubakaji 6,335, ulawiti 1,557 na mimba za utotoni 1,557 ambapo mikoa inayoongoza kwa matukio hayo ni Arusha matukio 728, Mbeya 710, mkoa wa kipolisi Kinondoni 681, Tanga 607 na Mwanza matukio 595.

Pia Dk Gwajima alisema wakati wa kuoneana aibu na kuacha adui aendelee kushambulia watoto umepitwa na wakati, hivyo jamii ivunje ukimya na kuondoa aibu katika kuripoti matukio ya ukatili kwa watoto kwani watu katili hutumia faida ya aibu na ukimya kuteka fahamu za watoto.

Waziri huyo pia alitoa mwito kwa familia kutumia siku hiyo kujadili changamoto na kutafuta suluhisho na majawabu ya namna ya kuendeleza amani na upendo ili kudumisha mshikamano katika familia na jamii kwa ujumla.

Pia aliwataka viongozi wa mikoa na halmashauri mbalimbali nchini kujihusisha kikamilifu katika maandalizi ya siku hiyo na wanatakiwa kushirikisha viongozi wa serikali na watu wa kawaida katika jamii.

Wanaotakiwa kushirikishwa ni pamoja na viongozi wa dini, mila, wazazi, walezi na watoto wenyewe ili wahusike katika mjadala ya malezi na makuzi ya watoto na mmomonyoko wa maadili unaoendelelea katika jamii.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Godwin Gondwe alisema wilaya yake inaungana moja kwa moja na Dk Gwajima kupinga na kutokomeza ukatili dhidi ya watoto kwani bila kufanya hivyo taifa la baadaye litapoteza nguvu kazi.

Habari Zifananazo

Back to top button