WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk Dorothy Gwajima ametoa wito kwa viongozi hususani wanawake kubeba ajenda ya kukabiliana na ukatili wa kijinsia na watoto kwenye vikao vyote kuanzia kwenye maeneo yao.
Dk Gwajima ametoa wito huo alipokuwa akiwasilisha mada ya mapambano ya ukatili dhidi ya wanawake na watoto kwenye mafunzo ya Wajumbe wa Jumuiya ya Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) na Viongozi wa UWT ngazi ya mikoa na wilaya jijini Dodoma leo Machi 21-22, 2023.
Amesema viongozi wanawake wana nafasi ya kuzungumzia ajenda ya kutokomeza ukatili wa kijinsia na kwa watoto kwani, pamoja na takwimu kuonesha wanawake wanafanyiwa ukatili, kuna baadhi ya wanawake wanakatili watoto au wanakatili wengine au wanajikatili wenyewe.
“Mila na Desturi nyingine zinatufanya tufanyiane ukatili wenyewe wanawake mfano
ukeketaji, kung’oa meno watoto, kuwafanyia urembo usio na tija watoto na kuwaumiza huku wengine kutovaa mavazi ya staha hivyo, umefika wakati wa kuongea haya kama tunahitaji kuleta mabadiliko ya ulimwengu huu” amesisitiza Dk Gwajima.
Dk Gwajima amefafanua kuwa wapo baadhi ya wazazi au walezi wanawasuka watoto nywele tena kwa maumivu makali urembo ambao hauna tija kwa watoto zaidi unawasababishia athari kwenye ubongo jambo ambalo ni ukatili wa Wanawake kwa watoto wa kike.
Amewahimiza viongozi hao kuhakikisha wanaweka mikakati kwenye jamii namna ya kupambana kutokomeza ukatili na malezi duni yanayochangia kuongezeka kwa vitendo vya ukatili huku akibainisha kuwa yanaleta athari za kimwili, kisaikolojia na kiuchumi.